Saturday, April 25, 2015

Shirika la Helvetas kutumia Bilioni 2.7 kuwezesha Wanawake wa Singida katika kilimo cha Mboga na matunda.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Helvetas Tanzania, Daniel Kilimbiya, akitoa mada yake ya utambulisho wa mradi wa awamu ya pili wa kuwawezesha wanawake kulima mboga mboga na matunda ili waweze kujikomboa kiuchumi. Semina hiyo iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Aqua Vitae mjini hapa, ilihudhurudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo kutoka wilaya ya Singida vijijini, Iramba na Mkalama.
Meneja SIDO mkoa wa Singida Shoma Kibende, akitoa nasaha zake kwenye semina ya siku moja ya uhabarisho wa mradi awamu ya pili unaolenga kuwawezesha wanawake kulima kilimo bora cha mboga mboga na matunda.

Kushoto ni kaimu mkuu wa mkoa wa Singida na DC wa wilaya ya Singida,Saidi Alli Kamanzi,akifuatilia mada zilizokuwa zikitolewa kwenye semina ya uhabarisho wa mradi wa awamu ya pili unaolenga kuwawezesha wanawake kulima kilimo bora cha mboga mboga na matunda.Wa pili kushoto ni mkuu wa wilaya ya Mkalama,Edward Ole Lenga.
Baadhi ya wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo waliohudhuria semina ya uhabarisho wa mradi awamu ya pili unaolenga kuwawezesha wanawake kulima kilimo bora cha matunda na mboga mboga.

SHIRIKA lisilo la kiserikali la Helvetas Tanzania  likishirikiana na SIDO mkoa wa Singida,linatarajia kutumia  zaidi ya shilingi 2.7 bilioni kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa mradi wa awamu ya pili wa kuwawezesha wanawake katika kilimo cha mboga mboga na matunda (KUWAKI), katika wilaya tatu ya mkoa wa Singida.

Fedha hizo zimetolewa na Jumuiya ya Umoja wa nchi za ulaya (European Union) na kwamba mradi huo umeanza kutekelezwa kuanzia januari mwaka huu na unatarajiwa kukamilika januari 12 mwaka 2018.

Hayo yamesemwa juzi na kaimu mkurugenzi mtendaji wa shirika la Helvetas Tanzania,Daniel Kilimbiya,wakati akitoa mada yake ya utambulisho wa mradi huo awamu ya pili kwenye semina ya siku moja iliyohudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo kutoka wilaya ya Singida vijijini,Iramba na Mkalama.

Alisema lengo kuu la mradi huo ni kuwawezesha wanawake kutumia fursa mbalimbali za kiuchumi,ili wawe na uhakika wa chakula katika kaya zao,na pia kupunguza unyanyasaji wa kijinsia katika kilimo.

“Ili kufikia lengo hili, vikundi vya wakulima vitafundishwa kilimo bora cha mboga mboga na matunda,vitapewa elimu ya kuweka na kukopa kwa njia ya kununua hisa,kusindika nyanya na mboga za majani.Vile vile watapewa elimu ya ujasiriamali na matumizi ya pampu za zege kwa ajili ya umwangiliaji mashamba yao”,alifafanua.

Kilimbiya alisema kuwa matarajio yao ni kwamba wazalishaji wadogo wadogo wa mboga mboga na matunda ambao ni wanawake na wanaume,watajengewa uwezo juu ya kilimo bora, ili kiwe na tija zaidi kwao kuliko ilivyo hivi sasa.

Alisema pamoja na kujengewa uwezo,pia mradi huo utasaidia kuongeza ushindani katika kilimo na kipato kupitia kilimo cha nyanya,vitunguu na mboga za majani katika vijiji 66 vilivyopo kata 15 za wilaya ya Mkalama,Iramba na Singida vijijini.

Katika hatua nyingine,Kilimbiya alisema katika awamu ya kwanza ya mradi huo iliyoanza kutekelezwa mwaka 2012 hadi mwaka jana katika wilaya za Mkalama,Ikungi,Iramba,Manispaa ya Singida na Singida vijijini,uliweza kufikia kaya 800 ambazo zilikuwa na vikundi 40 vya wakulima wanawake.

Alisema pamoja na mafanikio hayo,vile vile walikabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo ya uzalishaji hafifu na usiokuwa na tija unaosababishwa na uchumi mdogo.

Kaimu mkurugenzi huyo alitaja changamoto zingine kuwa ni ukosefu wa dhana za kisasa pamoja na kushindwa kwa wakulima wadogo kuwekeza katika teknolojia rahisi za kilimo cha mboga mboga na matunda.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Mkalama, Edward Ole Lenga,ametumia fursa hiyo kuwataka wakulima wa wilaya tatu za mradi huo,kuupokea kwa mikono miwili mradi huo na kushiriki kikamilifu utekelezaji wake,ili pamoja na mambo mengine,kaya ziweze kuwa na uhakika wa chakula kwa kipindi cha mwaka mzima.


“Wenzetu wa nchi za Jumuiya ya Umoja wa Ulaya wametuonea huruma na kutupa msaada wa fedha nyingi mno za mradi huu.Sasa msaada huu ni deni kwetu na kulilipa,ni sisi kujitahidi kufikia malengo yaliyowekwa”,alisisitiza Lenga.

No comments:

Post a Comment