Saturday, October 22, 2011

Ujenzi Wa Barabara Ya Singida-Katesh(Manyara), Wakamilika

Mkuu wa mkoa Dk.Kone, (kushoto) ba mhandisi Kkangolle(kulia),na wakandarasi wa wa ujenzi wa barabara hiyo iliyoigharimu serikali zaidi ya Sh.Bilioni 51.6, ambao umekamilika na magari yataruhusiwa kuanza kupita katika kipindi cha siku saba kuanzia leo.

Mkuu wa mkoa Dk.Kone, akipewa maelekezo na mhandisi Kangole, juu ya mawe mawili katika barabara hiyo, ambayo ni lango la kuingia na kutoka katika mji wa Singida

Mkuu wa mkoa Singida Dk.Parseko Kone(katikati), meneja wa wakala wa barabara Singida,mhandisi Yustak Kangole, wakiwa kwenye picha ya pamoja na wataalamu wa kampuni ya Sinohydro Corporation Ltd ya China, baada ya kukagua ujenzi wa barabara ya Singida-Kateshi(Manyara) kilomita 65.1

Mkuu wa mkoa Singida Dk.Parseko Kone baada ya kukagua mradi wa barabara ya Manyoni-Chaya, jana aliendelea na kazi hiyo, kwa kufanya ukaguzi barabara ya Singida-Kateshi(Manyara) inayojengwa na kampuni ya Sinohydro Corporation Ltd, kwa zaidi ya Sh.Bilioni 51.6.

Mkuu Wa Mkoa Wa Singida Akagua Ujenzi Wa Barabara Manyoni-Ch​aya(Tabora​)

Barabara hii ya Manyoni-Chaya(Tabora), ikijengwa kwa kasi,moja ya lori likionekana likimwaga mchanga kwenye barabara hiyo inayoigharimu serikali zaidi ya Sh.Bilioni 109.6, mradi huu unajengwa na kampuni ya Sinohydro,kutoka nchini China, wakati mkuu wa mkoa wa Singida Dk.Parseko Kone alipotembelea kujionea maendeleo yake

:Mkuu wa mkoa Singida Dk.Parseko Kone mwenye kofia ya bluu, akitaka ufafanuzi kwa mhandisi mshauri wa mradi wa barabara hiyo, kampuni ya Nicolous Odoya ya nchini Island,Bw. Patrick Gayer.

Mkuu wa mkoa wa Singida Dk.Parseko Kone akionyeshwa moja ya karo yanayotumika kuhifadhia maji kabla ya kutumiwa kwenye shughuli za ujenzi wa barabara hiyo yenye umbali wa kilomita 89.3, kutoka Manyoni(Singida) hadi Chaya(Tabora)

MKUU wa mkoa wa Singida Dk.Parseko Kone ameyataka makampuni yanayojishughulisha na kandarasi za ujenzi wa barabara, kukamilisha mapema miradi yao, ili kuendana sawa na mikataba wanayoingia na serikali.Dk.Kone ameyasema hayo leo, wakati akikagua mradi mkubwa wa ujenzi wa barabara ya Manyoni(Singida) hadi Chaya mkoani Tabora, kilomita 89.3, unaotekelezwa na kampuni ya SINOHYDRO,kutoka nchini China, kwa gharama ya zaidi ya Sh.Bilioni 109.6.
Hata hivyo aliipongeza kampuni hiyo kwa msingi wa barabara ambao mradi huo upo mbele kwa siku 53, lakini ameitaka kuchukua tahadhari wakati wa masika ambapo mvua huadhiri maendeleo ya ujenzi

Singida Kuzalisha Umeme Wa Upepo


Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Power Pool East Africa, Machwa Kagoswe akitoa maelezo kwa Naibu waziri wa Viwanda na Biashara, Lazaro Nyalandu juu ya eneo la kuzalishia umeme wa upepo mkoani Singida . Serikali imeingia Ubia kupitia Shiriaka la Maendeleo la Taifa (NDC) na kampuni binafsi ya Power Pool East Aftrica ili kuzalisha umeme huo kuanzia mwakani.

Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) limeingia ubia na kampuni ya Power Pool East Africa wa kuzalisha umeme wa upepo mkoani Singida utakaogharimu takribani ya Sh Bilioni 180.

Naibu waziri wa Viwanda na Biashara, Lazaro Nyalandu alisema tayari makubaliano yamesainiwa na shirika la NDC kwa niaba ya serikali itakuwa ikimiliki asilimia 51 za hisa na nyingine zitakuwa za mwekezaji binafsi.

Nyalandu alisema kwa mradi huo ambao utakuwa wa gharama nafuu katika uzalishaji utaingizwa katika gridi ya taifa na kwa kuanzia zitazalishwa megawati 50 na baadae zitaongezwa kulingana na uwezo wa wabia hao.

“Tokea kuanza kufungwa kwa mitambo itachukua takribani miezi 15 ili umeme uingie katika gridi na hii itakuwa ufumbuzi wa matatizo ya umeme kwa sasa” alisema Nyalandu.

Mkurugenzi wa Viwanda vikubwa wa NDC, Alley Mwakibolwa alieleza kuwa kwa ujenzi wa mitambo hiyo ya kutumia upepo kutasaidia kuzalisha umeme ampema kwani mitambo ya aina hiyo huchukua muda mfupi kuwekwa ikilinganishwa na ya maji ama ya gesi.

Tutajitahidi mradi huu uende kwa kasi kubwa kwani kwa kuanzia tutazalisha megawati 50 na baadae tutaongeza 50 ili kuoingia katika gridi ya taifa" alisema.

Aidha katikaeneo hilo ambalo liko ukingoni kwa bonde la ufa, upepo ni mkakli kiasi cha kufanya miti karibu yote kulalia upande mmoja na upeo huende kwa kasi ya hadi mita 21 kwa sekunde.

Friday, October 21, 2011

MWISHO WA KANALI GADAFFI


ALIYEKUWA kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi ameripotiwa kuuawa na wapiganaji wanaoongozwa na Baraza la Mpito nchini humo (NTC), baada ya mji wa nyumbani kwake, Sirte kunyakuliwa na vikosi hivyo jana.

Kifo cha Kanali Gaddafi (69) kilitangazwa rasmi na Waziri Mkuu wa Serikali ya mpito nchini humo, Mahmoud Jibril, muda mfupi baada kiongozi huyo aliyeitawala Libya kwa miaka 42 kuuawa.

Awali, msemaji wa NTC nchini Libya, Kanali Ahmed Bani alisema Kanali Gaddafi aliuawa na mwili wake ulipelekwa katika mji wa Misratah, bila kutoa ufafanuzi kamili kuhusu mazingira ya kifo hicho.

Taarifa za kuuawa kwake zilitolewa huku zikiambatanishwa na picha zinazoonyesha sura inayoonekana kuwa ni ya kiongozi huyo, katika muonekano wa nywele zake laini na ndefu wastani na uso uliotapakaa damu na majeraha.

Kanali Gaddafi anakuwa kiongozi wa kwanza kuuawa tangu kuanza vuguvugu la mageuzi katika mataifa ya kiarabu mwanzoni mwa mwaka huu, yaliyowaondoa madarakani Rais Ben Ali wa Tunisia na Hosni Mubarak wa Misri.

Kifo hicho kimetangazwa ikiwa ni miezi tisa tangu kuanza kwa upinzani mkali dhidi ya Serikali yake Februari mwaka huu, ambapo aliapa kwamba asingeondoka nchini Libya na kwamba yeye na wafuasi wake wangepambana hadi tone la mwisho la damu.

Kanali Gaddafi ambaye wakati wa utawala wake aliwahi kujipa wadhifa wa “mfalme wa wafalme wa Afrika” alikuwa akisifika kwa ukali wa sauti yake na maneno makali ya kuhamasisha na kueleza misimamo yake katika hotuba zake.

Mapambano hayo yameishia katika mji wa nyumbani kwake, Sirte ambao umekuwa na upinzani mkali kwa vikosi vya wapiganaji wa NTC ambavyo vililazimika kupambana kwa miezi kadhaa hadi waasi walipofanikiwa kuuteka jana.

Kanali Bani alisema mtoto wa Kanali Gaddafi, Mutassim ambaye walikuwa pamoja katika mji wa Sirte aliuawa na wapiganaji hao wa NTC.

Msemaji huyo aliwaambia waandishi wa habari kuwa kiongozi huyo alifariki dunia baada ya kujeruhiwa vibaya katika miguu yake yote na kichwani.

“Aliuawa katika mapambano na wapiganaji wetu. Kuna picha zinazoonyesha hayo,”alisema.

Alijificha kwenye karavati

Kwa mujibu wa taarifa za vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa, Kanali Gaddafi alidhibitiwa baada ya kukutwa amejificha katika karavati la barabarani, yeye pamoja na baadhi ya walinzi wake.

Kwa upande wake, kamanda wa wapiganaji wa baraza hilo, Abdul Hakim Belhaj pia alithibitisha kuwa Kanali Gaddafi alifariki dunia kutokana na majeraha aliyoyapata baada ya kukamatwa.

Makamu Mwenyekiti wa NTC, Abdul Hafiz Ghoga alithibitisha mbele ya waandishi wa habari kuwa Gaddafi aliuawa katika mji wa Sirte.

“Tunatangaza kwa dunia kuwa Muammar Gaddafi aliuawa katika mikono ya wanamapinduzi,” alisema Ghoga.

Katika mtiririko wa matukio yaliyokuwa yakirushwa katika vituo mbalimbali vya televisheni, kituo cha televisheni cha al-Jazeera kilionyesha picha za mwili wa Kanali Gaddafi ukiburuzwa katika eneo alilouawa.

Filamu za video zilizochukuliwa kwa simu za mkono zilionyesha kile kilichoonekana kuwa maiti ya Gaddafi iliyolowa damu. Mwili wake baadaye uliburuzwa na wapiganaji na kupakiwa nyuma ya gari aina ya pick-up.


Nato na Marekani zilieleza kuwa haziwezi kuthibitisha taarifa za kuuwawa kwa kiongozi huyo ambaye hajaonekana tangu NTC ilipoikamata Tripoli.

Watu washangilia mitaani

Wakati huohuo, katika mji wa Benghazi na miji mingine nchini humo, watu walionekana kukusanyika mitaani na kushangilia taarifa hizo za kuuawa kwa Gaddafi.

Viongozi mbalimbali duniani pia wamezungumzia kuhusu taarifa hizo za kuuawa kwa Kanali Gaddafi ambaye amewahi kuwa mpinzani mkubwa wa mataifa ya Ulaya na Marekani kutokana na misimamo yake dhidi ya mataifa hayo.

Miongoni mwa viongozi hao ni Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameroon ambaye alisema ni siku maalum ya kukumbuka maovu yote yaliyofanywa na Gaddafi.

Alisema watu wa Libya wako katika nafasi nzuri ya kujenga nchi imara na yenye demokrasia.

“Ninafurahi kazi ambayo Uingereza imesaidia katika kuuondoa utawala wa Gaddafi,”alisema.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Alain Juppe amepongeza kufikiwa mwisho kwa utawala wa miaka 42 ya Gaddafi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon pia alisema kwamba kifo cha Kanali Gaddafi kinatoa mwanya wa “historia mpya kwa Libya”.

“Watu wanatakiwa watambue kuwa huu ni mwisho wa mwanzo. Sasa ni wakati wa Walibya wote kushikamana na kuwa kitu kimoja. Ni wakati wa kuponya majeraha na kujenga upya taifa. Si wakati wa visasi,” alisema Ki-Moon.

Balozi wa Libya nchini Uingereza, Mahmud Nacua alisema kuwa kuawa kwa Gaddafi kunamaanisha Libya inaelekea kwenye mustakhabali bora wa baadaye.

Wasifu wa Kanali Muammar Gaddafi

Alikuwa mtoto wa wafugaji wa Kibedui, mwenye maisha ya utata, lakini ambaye alitukuzwa sana, huku mataifa ya Magharibi yakimuona mtu wa hatari wakati wote.

Muammar Muhammad Gaddafi aliitawala Libya kwa zaidi ya miaka 40. Hadi mwanzoni mwa Machi 2011, alikuwa akiamini ndani ya moyo wake kwamba watu wake walikuwa wakimpenda na kwamba walikuwa tayari kumlinda hadi kufa kwa ajili yake.

Lakini wakati huo, tayari Gaddafi alikuwa ameshatumia njia za kikatili kuyazima maandamano dhidi yake, maandamano ambayo baadaye yaligeuka vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Kwa mujibu wa taarifa, watu zaidi ya 30,000 waliuawa kwenye vita hivyo. Mara nyingi sana, Gaddafi alitoa matamko makali wakati wa vita hivyo, ila linalojuilikana zaidi ni lile la kuwaita wapinzani wake kuwa ni panya.

Kwa kila hali, yaliyotokea ni mambo ambayo Gaddafi hakuyatarajia asilani. Mtoto huyu wa wafugaji wa Kibedui aliyezaliwa mwaka 1942, alikuja kuibuka kama mkombozi wa Walibya, alipompindua Mfalme Idriss hapo mwaka 1969.

Kuanzia hapo akaanza kujenga kile alichokiona mwenyewe kuwa ni mfumo wa kidemokrasia wa moja kwa moja. Alianzisha kamati za umma zilizoamua juu ya mustakabali wa umma na wa Serikali. Aliuita mfumo wake wa kisiasa na kiuchumi kuwa ni wa kisoshalisti, alioufafanua kwenye kijitabu chake cha Kijani.

Historia yake kiufupi

Alizaliwa mwaka 1942 katika eneo la Jangwa, kwenye mji wa Sirte, katika familia ya baba Mohamed Abdulsalama Abuminiar na mama Aisha Ben Niran. Alijiunga na Jeshi la Libya mwaka 1965.
Alifanya mapinduzi ya Serikali yasiyo ya umwagaji damu na kumuondoa mfalme Idris katika utawala wake mwaka 1969 na kuwa mtawala wa Libya akiwa na umri wa miaka 27.

Alikuwa maarufu kwa nguo anazopenda kuvaa na walinzi wa kike wenye kubeba silaha, kiongozi huyo wa Libya pia anadhaniwa kuwa na mbinu nzuri za kisiasa kwa kuweza kuirejesha Libya kutokana na kutengwa kidiplomasia duniani.

Baada ya miongo miwili ya kutengwa katika jamii ya kimataifa, mwaka 2003, Tripoli ilikiri kuwa walifanya shambulio la Lockerbie kwa kuiangamiza kwa mabomu ndege ya Pam Am. Umoja wa Mataifa (UN) ulikubali kuondoa vikwazo dhidi ya Libya.



Baada ya miezi kadhaa, Serikali ya Kanali Gaddafi ilisitisha mipango yake ya kuunda silaha za maangamizi na hii ikarejesha ushirikiano na nchi za Magharibi.

Gaddafi ni mtu wa kipekee katika kauli zake, mienendo yake, tabia zake na mikakati yake, kwa mujibu wa Saas Djebbar, mtaalam wa siasa za Libya.
Alipokuwa kijana alivutiwa na kiongozi mzalendo wa Misri, Gamal Abdel Nasser, alipokuwa akishiriki katika maandamano dhidi ya Israel wakati wa mtafaruku wa Suez mwaka 1956.

Alipanga njama ya kupindua utawala wa kifalme alipokuwa mwanafunzi wa kijeshi alipokuwa mafunzoni Uingereza kabla ya kurejea nyumbani Libya. Alipanga mapinduzi ya Septemba 1, 1969 akiwa katika mji wa Benghazi.

Alianza kujenga itikadi zake za kisiasa mwaka 1970 na kuziandika katika kitabu chake cha kijani kibichi.
Alikitumia kitabu chake kuanzisha mfumo wa kisiasa uliojumuisha kanuni za Kiislamu na mfumo ulio tofauti na siasa za ujamaa au ubepari.

Mwaka1977 aliasisi mfumo ujulikanao kama 'Jamahiriya' au 'Taifa la Umma' ambapo raia ndio wanaoendesha uongozi wa nchi yao kupitia 'kamati za umma'.

Mfumo huo wa Gaddafi umevuka mipaka na hauhusishi mambo ya siasa tu, bali pia mambo mengine.
Akiwa safarini ng'ambo, alikuwa akitumia makazi maalum kwenye kambi iliyojengwa na hema yake ya kifahari ya Kibeduwi akiwa amefuatana na walinzi wanawake ambao, inasemekana, huwa hawapotezi umakini kazini kama walinzi wanaume.Hema hiyo pia ilitumiwa kuwalaki wageni wa Libya na Kanali Gaddafi huendesha mikutano na mahojiano yake humo humo akipepea usinga au tawi la mitende.

Rais wa zamani wa Marekani Ronald Reagan alimwita Gaddafi 'mad dog' yaani 'mbwa kichaa' na Marekani ililipiza kisasi dhidi ya Libya kwa madai ya kuhusika na mashambulio ya anga barani Ulaya kwa kuvamia miji ya Tripoli na Benghazi mwaka 1986.Aliposhindwa katika jitihada zake za kuzipatanisha nchi za Uarabuni katika miaka ya 90, Kanali Gaddafi alielekeza nguvu zake barani Afrika na kupendekeza 'Muungano wa Nchi' za bara la Afrika.

Alianza kuvaa mavazi yake binafsi, sare za michezo zilizo na ngao za Bara la Afrika au picha za viongozi kutoka bara hilo.Aliwahi kuvunja na kufuta Wizara za nchi hiyo pamoja na bajeti zao, isipokuwa Wizara chache ikiwemo ya Ulinzi, Fedha na Mambo ya Nje.Licha ya uchumi wa Libya kutoa fursa kwa wawekezaji wa nje, mabadiliko bado yanakwenda taratibu.

Vuguvugu la mageuzi dhidi yake lilipoanza mwanzoni mwa mwaka huu, aliapa kuwafuata wanaompinga nyumba hadi nyumba, mlango kwa mlango, hatua iliyoibua hasira na kuchochea harakati za kijeshi dhidi yake.

Baada ya baadhi ya askari kutangaza kujitoa katika jeshi lake na kuanzisha uasi, aliapa kwamba atapambana hadi tone la mwisho la damu litakapomwagika. Alisisitiza kwamba kamwe hatakimbia kutoka katika ardhi ya Libya, atafia katika ardhi ya mababu zake.

Taarifa zilieleza jana kwamba aliuawa baada ya kukutwa akiwa amejificha katika daraja dogo kwa ajili ya kupitisha maji barabarani (karavati).

Mara baada ya kuuawa, wapiganaji wa Baraza la Mpito waliokuwa katika mapambano dhidi yake walibaini kwamba alikuwa na bastola iliyotengenezwa kwa dhahabu tupu.

JK aahidi kukiboresha UDSM


SERIKALI imeahidi kukiboresha Chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na makazi ya wafanyakazi ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa chuo hicho.Uboreshwaji huo utakuwa ni pamoja na ujenzi wa hosteli katika kampasi kuu itakayokuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 4,500 na nyumba 450 za watumishi wa chuo hicho.

Akizungumza katika maadhimisho hayo yaliyokwenda sambamba na sherehe za mahafali ya 41 yaliyofanyika katika Ukumbi wa Nkrumah, Rais Jakaya Kikwete alisema uamuzi huo ni moja ya mipango ya Serikali kuboresha vyuo vikuu nchini.

Rais Kikwete ambaye aliambatana na Rais Yoweri Museveni ambaye aliwahi kusoma chuoni hapo miaka ya nyuma, alisema "nimeambiwa hali ya makazi ni mbaya inayohitaji hatua za haraka. Tutaliangalia hilo".

Kwa mujibu wa Rais, "Serikali pia itakisaidia chuo kutekeleza mpango wake wa ujenzi wa nyumba 450 kwa ajili ya watumishi wake".

Alisema serikali pia inakaribisha na itasaidia ujenzi wa kituo cha wanafunzi kwa ajili ya kujisomea na kuongeza, " Kama nyote mnavyojua, mimi na kaka yangu Rais Museveni tumeshiriki katika juhudi mbalimbali kufanikisha fedha za mradi huo".


Mpango wa elimu ya juu
Akizungumzia Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Juu (HEDP), Rais Kikwete alisema umeandaliwa kwa kipindi cha miaka mitano kutoka 2010 hadi 2015 na kila mwaka utakuwa ukigharimu Serikali Sh52bilioni.

Alisema HEDP una malengo makuu matano ambayo ni pamoja na kutoa mafunzo ya muda mfupi na mrefu kwa watumishi, kujenga miundo mbinu iliyopo na kujenga mipya, kutoa vifaa vya kufundishia na kujisomea ambavyo ni pamoja na vitabu na kompyuta.

Lengo jingine alilotaja Rais, ni pamoja na matumizi ya teknoloji ya kisasa ya Mawasiliano kwa Kompyuta (ICT) na kufanya tafiti na uwezeshaji wake.

Alisema ni dhamira ya Serikali kuona sekta binafsi inashiriki vema katika kujenga vyuo vikuu zaidi katika nchi na kuongeza kwamba, "tutaendelea kupanua wigo wa upatikanaji mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu".

Kwa mujibu wa Rais, mwaka 2005/06 mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu ilikuwa ni Sh56.1 bilioni lakini hadi kufikia mwaka huu mikopo hiyo imeongezeka na kufikia kiasi cha Sh317.9 bilioni na kusisitiza, "hii inatuwezesha kuongeza namba ya wanafunzi wanaopata udhamini wa Serikali kupata mikopo kutoka 16,345 kati ya mwaka 2005/06 hadi kufikia 93,105 mwaka huu".

Rais alizidi kujivunia mafanikio akisema, idadi ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza watakaopata mikopo kwa mwaka huu ambayo ni 24,625 ni kubwa ya idadi jumla ya wanafunzi wote wa vyuo vikuu kwa mwaka 2005

Alisema kuwa kumekuwa na ongezeko la uandikishwaji wa wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka 42,948 mwaka 2004 hadi 95,525 mwaka 2009.

Museveni
Katika hatua nyingine Rais wa Uganda, Yoweri Mseveni aliwapongeza waanzilishi wa chuo hicho na kusema,
“Tanzania inastahili pongezi nyingi sana, kwani Mwanasheria Mkuu wa nchi yangu hajasoma Uingereza wala India bali ni matunda ya Chuo hiki,”.

Alisema yeye pia ni matunda ya chuo hicho na bado kinaendelea kuisaidia Uganda kwa kupokea wanafunzi wake.

“Sisi na watanzani wote tunapaswa kujivunia UDSM na tuhakikishe kinaendelea kwani katika miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania kimekuwa ni msaada kwa maendeleo ya nchi mbalimbali” alisema Rais huyo mwenye kupenda kuvaa kofia pana.

MADUKA MANNE YAUNGUA MOTO MJINI SINGIDA



Dogo akiwa kwenye hekaheka


Picha zote tatu zikionyesha jinsi maduka yalivyokua yakiteketea kwa moto
Watu wakiwa katika harakati za kuokoa vitu vyoa

Gari la zima moto likifanya kazi yake

Hali hilivyokua baada ya moto kuzimwa nusu na kikosi cha zima moto.
Hakuna mtu aliyepoteza maisha au kujeruhiwa

EPIC NATION NDANI YA SINGIDA

GARI LA MADEE NA DOGO JANJA LIKIINGIA NAMFUA HUKU LIKISINDIKIZWA NA WASHABIKI WAO

WANA WENGINE WAKISINDIKIZA SHANGWE ZA EPIC NATION NDANI YA SINGIDA

MADEE NA DOGO JANJA WALIPO PANDA STAGENI




WAKAZI MBALIMBALI WA SINGIDA WAKISHUHUDIA SHAGWE ZA EPIC NATION


MADEE NA DOGO JANJA WALIVYO ZONGWA BAADA YA KUSHUKA STAGENI
KWA MBALI NI GARI LA MADEE NA DOGO JANJA LIKIKIMBIZWA NA MASHABIKI WAO LILIPOKUWA LIKIONDIKA