Friday, October 21, 2011

JK aahidi kukiboresha UDSM


SERIKALI imeahidi kukiboresha Chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na makazi ya wafanyakazi ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa chuo hicho.Uboreshwaji huo utakuwa ni pamoja na ujenzi wa hosteli katika kampasi kuu itakayokuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 4,500 na nyumba 450 za watumishi wa chuo hicho.

Akizungumza katika maadhimisho hayo yaliyokwenda sambamba na sherehe za mahafali ya 41 yaliyofanyika katika Ukumbi wa Nkrumah, Rais Jakaya Kikwete alisema uamuzi huo ni moja ya mipango ya Serikali kuboresha vyuo vikuu nchini.

Rais Kikwete ambaye aliambatana na Rais Yoweri Museveni ambaye aliwahi kusoma chuoni hapo miaka ya nyuma, alisema "nimeambiwa hali ya makazi ni mbaya inayohitaji hatua za haraka. Tutaliangalia hilo".

Kwa mujibu wa Rais, "Serikali pia itakisaidia chuo kutekeleza mpango wake wa ujenzi wa nyumba 450 kwa ajili ya watumishi wake".

Alisema serikali pia inakaribisha na itasaidia ujenzi wa kituo cha wanafunzi kwa ajili ya kujisomea na kuongeza, " Kama nyote mnavyojua, mimi na kaka yangu Rais Museveni tumeshiriki katika juhudi mbalimbali kufanikisha fedha za mradi huo".


Mpango wa elimu ya juu
Akizungumzia Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Juu (HEDP), Rais Kikwete alisema umeandaliwa kwa kipindi cha miaka mitano kutoka 2010 hadi 2015 na kila mwaka utakuwa ukigharimu Serikali Sh52bilioni.

Alisema HEDP una malengo makuu matano ambayo ni pamoja na kutoa mafunzo ya muda mfupi na mrefu kwa watumishi, kujenga miundo mbinu iliyopo na kujenga mipya, kutoa vifaa vya kufundishia na kujisomea ambavyo ni pamoja na vitabu na kompyuta.

Lengo jingine alilotaja Rais, ni pamoja na matumizi ya teknoloji ya kisasa ya Mawasiliano kwa Kompyuta (ICT) na kufanya tafiti na uwezeshaji wake.

Alisema ni dhamira ya Serikali kuona sekta binafsi inashiriki vema katika kujenga vyuo vikuu zaidi katika nchi na kuongeza kwamba, "tutaendelea kupanua wigo wa upatikanaji mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu".

Kwa mujibu wa Rais, mwaka 2005/06 mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu ilikuwa ni Sh56.1 bilioni lakini hadi kufikia mwaka huu mikopo hiyo imeongezeka na kufikia kiasi cha Sh317.9 bilioni na kusisitiza, "hii inatuwezesha kuongeza namba ya wanafunzi wanaopata udhamini wa Serikali kupata mikopo kutoka 16,345 kati ya mwaka 2005/06 hadi kufikia 93,105 mwaka huu".

Rais alizidi kujivunia mafanikio akisema, idadi ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza watakaopata mikopo kwa mwaka huu ambayo ni 24,625 ni kubwa ya idadi jumla ya wanafunzi wote wa vyuo vikuu kwa mwaka 2005

Alisema kuwa kumekuwa na ongezeko la uandikishwaji wa wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka 42,948 mwaka 2004 hadi 95,525 mwaka 2009.

Museveni
Katika hatua nyingine Rais wa Uganda, Yoweri Mseveni aliwapongeza waanzilishi wa chuo hicho na kusema,
“Tanzania inastahili pongezi nyingi sana, kwani Mwanasheria Mkuu wa nchi yangu hajasoma Uingereza wala India bali ni matunda ya Chuo hiki,”.

Alisema yeye pia ni matunda ya chuo hicho na bado kinaendelea kuisaidia Uganda kwa kupokea wanafunzi wake.

“Sisi na watanzani wote tunapaswa kujivunia UDSM na tuhakikishe kinaendelea kwani katika miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania kimekuwa ni msaada kwa maendeleo ya nchi mbalimbali” alisema Rais huyo mwenye kupenda kuvaa kofia pana.

No comments:

Post a Comment