Friday, September 6, 2013

Wadau wa Ukimwi washauriwa kuongeza juhudi kwenye mapambano dhidi ya Ukimwi

 Afisa Ustawi wa Jamii katika Sekretarieti ya mkoa wa Singida, Zuhura Karya (kulia) akizungumza kwenye ufunguzi wa semina ya wadau wa vita dhidi ya UKIMWI wa wilaya ya Ikungi.Wa kwanza kushoto ni mratibu wa vita dhidi ya UKIMWI katika wilaya ya Ikungi, Mussa na wa pili kushoto ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Ikungi, Selestin Yunde. Semina hiyo imefanyika katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha maendeleo ya wananchi mjini Singida.
 Baadhi ya wadau wa vita dhidi ya UKIMWI wa wilaya ya Ikungi mkoa wa Singida,wakifuatilia kwa makini semina ya siku moja iliyohusu kujadiliana na kuweka mikakati ya kumaliza kabisa maambukizi mapya ya VVU.Semina hiyo imefanyikia kwenye ukumbi wa mikutano wa chuo cha maendeleo ya wananchi mjini Singida.

Wadau wa vita dhidi ya Ukimwi Wilayani Ikungi wametakiwa kutobweteka na kitendo cha kupungua kwa maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi na badala yake waongeze kazi ya kupambana na ugonjwa  huo ili ifikapo mwaka 2015 maambukizi, unyanyapaa na vifo vifikie asilimia sifuri.

Changamoto hiyo imetolewa juzi na Afisa Ustawi wa Jamii Sekretarieti ya Mkoa wa Singida,Zuhura Kyara,wakati akifungua mkutano wa wadau wa UKIMWI katika wilaya mpya ya Ikungi uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Chuo Cha Maendeleo ya wananchi mjini hapa.

Alisema maambukizi mapya ya VVU katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida na Ikungi,takwimu zinaonyesha kuwa yamepungua kutoka asilimia nne hadi mbili mwaka huu.

Kyara alisema hayo ni mafanikio mazuri lakini hata hivyo,juhudi zaidi zinapaswa kuongezwa ili kufikia mwaka
2015,pasiwepo kabisa na maambukizi mapya,unyanyapaa na vifo vitokanavyo na UKIMWI kama dunia ilivyoazimia.

“Dira na maono yetu kama wadau,ni kuhakikisha tunaweka misingi imara yenye mwelekeo wa kutimiza azma hii.Hivyo tutumie fursa hii ya mkutano huu kufanya majadiliano juu ya mikakati ya kukabili changamoto  mbalimbali za VVU/UKIMWI”,alifafanua Karya.

Afisa huyo alitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni kupunguza maambukizi ya VVU kwa vijana  yanayosababishwa na ngono zembe kama sehemu ya kujipatia kipato.

Karya alitaja changamoto zingine kuwa ni kupunguza vifo vyote vinavyosababishwa na ugonjwa wa kifua kikuu na kuhakikisha upatikanaji wa dawa za kufubaza VVU kwa watu wote wanaoishi na VVU na kupatiwa matibabu yote wanayostahili kupewa.

No comments:

Post a Comment