Monday, July 21, 2014

Utoaji elimu ya afya ya uzazi na ujinsia wafanikiwa.

Mratiibu msaidizi wa polisi mkoa wa Singida,Irene Mbwatila,(anayeangalia kamera),akizungumza na timu ya pamoja ya maafisa wa shirika la HAPA,YMC na RFSU, inayofanya utafiti juu ya mradi wa ushiriki sawa wa wanaume katika afya ya uzazi na ujinsia.
Baadhi ya wanaume wakiwa na wake zao wakazi wa kijiji cha Ntuntu wilaya ya Ikungi mkoa wa Singida, wakiwa kwenye foleni katika kliniki ya kijijini hapo,wakisubiri kuingia kumwona muuguzi. Elimu iliyotolewa kwa pamoja na mashirika ya HAPA na YMC,ya umuhimu wa ushiriki sawa wa wanaume katika afya ya uzazi na unjisia, katika kipindi cha miaka mitatu, imechangia wanaume pamoja na mambo mengine, kusindikiza wake zao kliniki kutoka asilimia 0 hadi 80 ya sasa.
Muuguzi wa zahanati ya kijiji cha Ntuntu wilaya ya Ikungi mkoa wa Singida, Mary Lema, akitoa dawa kwa mama mjamzito Lucia Hongoa, huku mume wake Edward akiwa anashuhudia. Kijiji cha Ntuntu ni moja ya vijiji ambavyo elimu ya ushiriki sawa wa wanaume katika afya ya uzazi na ujinsia,inatolewa.
Muuguzi wa zahanati ya kijiji cha Ntuntu wilaya ya Ikungi mkoa wa Singida, Mary Lema akitoa taarifa yake juu ya utekelezaji wa mradi wa ushiriki sawa wa wanaume katika afya ya uzazi na ujinsia kwa waandishi wa habari (hawapo pichani).

 ELIMU ya ushiriki sawa wa wanaume katika afya ya uzazi na ujinsia inayotolewa kwa pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali ya HAPA na YMC imezaa matunda baada ya wanaume kubadilika, na kuanza kusindikiza wake zao klinki na kusaidia kazi zote za nyumbani,imeelezwa.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, muuguzi wa kliniki ya zahanati ya kijiji cha Ntuntu wilaya ya Ikungi mkoa wa Singida, Mary Lema, amesema kuwa miaka mitatu iliyopita,hakukuwa na mwanaume anayesindikiza mke wake klinki.

Alisema elimu hiyo imewahamasisha na kuwaelimisha wanaume ambao kwa sasa
wanashiriki kikamilifu, afya ya uzazi na ujinsia kutoka asilimia 0 hadi 80.

Lema amesema kuwa kwa sasa kama mwanaume hajamsindikiza mke wake mjamzito kliniki,atafanya hivyo kwa sababu za msingi.

“Kwa kawaida wanaume wakazi wa wilaya hii na mkoa kwa ujumla,huwa ni mwiko kusindikiza mke kliniki au kufanya kazi zingine za nyumbani kama kufua nguo,kupika,kuchota maji na kusenya kuni.Lakini baada ya elimu hii ya ushiriki sawa wa wanaume katika afya ya uzazi na ujinsia kutolewa,wanaume karibu wote,wamebadilika”,alifafanua.

Akifafanua zaidi,alisema kuwa wanaume karibu wote wa kijiji cha Ntuntu kwa sasa wanafanya/wanashiriki  shughuli zote za nyumbani sawia na wanawake,kitendo kinachoboresha sana mahusiano na mapenzi.

Kwa upande wake Ana Charles, amesema kuwa baada ya elimu hiyo kutolewa kijijini hapo, wanaume wamebadilika mno kwa kuwa wapole, kuwahi kurudi nyumbani na mapenzi yameboreka zaidi.


“Kwa sasa wanaume wetu wamejenga tabia ya kuambatana nasi kwenda kupata moja baridi kitendo ambacho hakikuwepo miaka mitatu iliyopita.Pia wamekuwa wapole hatupigwi ovyo kama ilivyokuwa zamani”,amesema Ana huku akitambasamu.

No comments:

Post a Comment