Saturday, August 31, 2013

Mh. Dewji atoa vifaa vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 10 kukuza soka mkoani Singida.

 Mgeni rasmi katika hafla ya kukabidhi vifaa vya mchezo wa soka Katibu wa mwenezi wa CCM Singida mjini Jumanne Rajabu (kushoto) akimkabidhi vifaa hivyo mmoja wa viongozi wa kata za jimbo la Singida kwa ajili ya maandalizi ya ligi ya kombe la MO inayotarajiwa kuanza mwezi Septemba mwaka huu.
 Katibu wa mbunge wa jimbo la Singida mjini Mh. Mohammed Gullam Dewji, Duda Mughenyi, akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi msaada wa vifaa vya mchezo wa soka vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni kumi, vilivyotolewa na Mh. Dewji. Vifaa hivyo vitatumika kwenye ligi ya kombe la MO inayotarajiwa kuanza rasmi Septemba mosi mwaka huu uwanja wa Namfua.
 Mgeni rasmi wa hafla ya kukabidhi vifaa vya mchezo wa soka, Katibu mwenezi wa CCM manispaa ya Singida Jumanne Rajabu, akizungumza muda mfupi kabla hajakabidhi vifaa hivyo.
 Katibu wa uchumi wa CCM jimbo la Singida mjini Moleli, akitoa nasaha zake kwenye hafla ya kukabidhi vifaa vya mchezo wa soka vilivyotolewa msaada kwa timu 16 za soka zitakazoshiriki ligi ya MO.
Baadhi ya vifaa vya mchezo wa soka vilivyotolewa msaada na mbunge wa jimbo la Singida mjin Mh. Mohammed Gullam Dewji kwa ajili ya ligi yake.

Mbunge wa jimbo la Singida mjini Mh. Mohammed Gullam Dewji, ametoa msaada wa vifaa mbalimbali vya mchezo wa soka vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni kumi.

 Vifaa hivyo vitatumika kwenye ligi ya kombe la mbunge Dewji maarufu kwa jina la MO ,inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Septemba mosi mwaka huu.

 Akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi vifaa hivyo, Katibu wa mbunge Dewji, Duda Mughenyi, amesema vifaa hivyo ni kwa ajili ya matumizi ya timu 16 za soka za kata za jimbo la Singida mjini.

 Ametaja vifaa hivyo kuwa ni
mipira 48, jezi 240, soksi 240 na glovu 16 za walinda magoli (golikipa).

Kwa upande wake mgeni rasmi katika hafla hiyo, Katibu mwenezi wa CCM jimbo la Singida mjini Jumanne Rajabu, amewataka wachezaji kujiunga katika vikundi vya kuweka na kukopa (SACCOS) ili kujijengea mazingira mazuri ya kukopesheka na taasisi za fedha yakiwemo mabenki.

 Amesema katika vikundi licha ya kuwa kwenye nafasi nzuri ya kukopesheka, pia vinavutia wafadhili/wahisani  kuvisaidia misaada mbalimbali.

 Aidha, Jumanne amewataka vijana watakaobahatika kushiriki kwenye ligi hiyo ya Mo, kujiwekea malengo ya kufika mbali kwenye mchezo wa soka wenye nafasi tele za kujiajiri na kuajiriwa.


 Jumanne ametumia fursa hiyo kumpongeza Dewji kwa uamuzi wake wa kuwapa nafasi vijana kuonyesha vipaji vyao kwenye mchezo wa soka unaopendwa zaidi duniani.

No comments:

Post a Comment