Thursday, August 22, 2013

Wito watolewa kwa waandishi wa habari kushirikiana na Wataalam wa Afya kufanya tafiti ili kuboresha sekta ya Afya nchini.

 Mwezeshaji wa mafunzo ya masuala ya Afya waJjumuiya ya vilabu vya waandishi wa habari nchini (UTPC),Dk.Ahmed Twaha (wa pili kulia) akitoa wito kwa waandishi wa habari (hawapo kwenye picha) kushirikiana na Wataalam wa Afya kufanya tafiti katika masuala ya Afya zitakazosaidia kuboresha Sekta ya Afya. Dk.Twaha ametoa wito huo kwenye kikao kifupi kati ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk.Dorothy Gwajima na waandishi wa habari.
 Mganga mkuu wa mkoa wa Singida, Dk.Dorothy Gwajima akitoa ufafanuzi wa masuala ya Afya kwa Waandishi wa Habari (hawapo kwenye picha) waliomtembelea ofisini kwake.
Baadhi ya waandishi wa habari waliohudhuria kikao kati yao na mganga mkuu wa mkoa wa Singida Dk.Dorothy Gwajima kilichofanyikia ofisini kwa mganga mkuu huyo.

Wanachama wa klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Singida, wameshauriwa kushirikiana na wataalam wa Afya kufanya tafiti mbalimbali zitakazosaidia kudhibiti/kutokomeza magonjwa ambayo ni kero kwa wananchi.
Changamoto hiyo imetolewa na mwezeshaji wa masuala ya Afya Dk.Ahmed Twaha wakati akizungumza kwenye kikao kifupi kati ya Mganga Mkuu wa mkoa wa Singida na waandishi wa habari.

Amesema vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika mapambano dhidi ya adui maradhi kama vikitumika ipasavyo.

“Mkitumia vizuri kalamu zenu katika kuielimisha jamii kupitia Redio, Tv au Makala katika magazeti juu ya athari mbalimbali zinazosababishwa na maradhi itasaidia jamii kuchukua hatua za kujihadhari na magonjwa na kwa ujumla na mtakuwa mmeusaidia Mkoa kuwa na wakazi wenye Afya bora”,amesema.

Pia amewataka kujenga utamaduni wa
kujielimisha juu ya maradhi mbalimbali ili kuwa na uelewa mpana ambao utaondoa uwezekano wa kupotosha jamii.

Kwa upande wake mganga mkuu wa mkoa, Dk.Dorothy Gwajima ameahidi kuwa karibu na waandishi wa habari ili pamoja na mambo mengine wakazi wa mkoa wa Singida waweze kujua ni nini kinachofanyika ndani ya sekta ya Afya mkoani mwao.


“Mimi naamini kwamba waandishi wa habari wako karibu zaidi na jamii hivyo kufanya kazi na ninyi kutaongeza ufanisi zaidi katika utoaji wa huduma ya afya”,amesema Dk.Gwajima.

No comments:

Post a Comment