Saturday, August 31, 2013

Kijana aliyeua akimuokoa mama yake asibakwe aachiwa huru na mahakama kuu kanda ya Dodoma.

Mahakama kuu Kanda ya Dodoma inaendelea na vikao vyake mjini Singida, imemwachia huru kijana  Elikana Selemani (28) mkazi wa kijiji cha Sefunga wilaya ya Singida vijijini, baada ya kukiri kosa la kumuuwa Omari Muna bila kukusudia.

Imedaiwa kuwa Elikana alitenda kosa hilo la mauaji, wakati akimuokoa mama yake mzazi asibakwe na kina Omari Muna.

Mapema mwendesha mashitaka mwanasheria wa serikali Masanja, alidai mbele ya Jaji Rehema Mkuye, kuwa mnamo Januari 31 mwaka jana saa 4:00 asubuhi huko katika kijiji cha Sefunga wilaya ya Singida vijijini, mshitakiwa Elikana alimpiga fimbo moja kichwani Omari Muna na kusababisha kifo chake baada ya siku mbili.

Masanja alisema siku ya tukio, mshtakiwa Elikana akiwa nyumbani kwao, alisikia yowe kutoka kwa  mama yake mzazi akiomba msaada kutoka ndani ya shamba lao la mahindi.

Alisema Elikana akiwa amebeba fimbo, alipofika eneo la tukio, alishuhudia Omari Muna, akiwa amemlalia  juu mama yake........
akitaka kumbaka.

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, mwendesha mashitaka Masanja, aliiomba mahakama hiyo itoe adhabu kwa mshitakiwa kadri itakapoona inastahiki.

Kwa upande wake wakili wa mshitakiwa  Raymond Kimu, aliiomba mahakama hiyo, impe mteja wake adhabu nafuu kwa kuzingatia kuwa ni kijana pekee anayetegemewa na mama yake mzazi.

Masanja alisema “Pia marehemu Omari amechangia kifo chake ,kwa kitendo chake kiovu cha kutaka kumbaka mwanamke mwenye umri sawa na wa mama yake”.

Aidha, alisema  mama yake pia anataka kumwona Elikana ili pengine ataacha kufikiria kitendo cha kinyama alichotaka kufanyiwa.

Akitoa hukumu hiyo, Jaji Mkuye alisema mshitakiwa ni kijana anayetegemewa na mama yake na vile vile toka siku ya kwanza ameendelea kutoa ushirikiano kwa kukiri kosa la mauaji hadi mahakama kuu.

Hili jambo ni baya sana na kwa vyo vyote litamsumbua maisha yake yote.

Amesema hata mama yake Elikana tukio hilo la kuta kubaka kushuhudiwa na mtoto wake, pia litamsumbua maisha yake yote yaliyobaki.

Jaji Mkuye amemwambia kijana huyo “Kwa hali hiyo, mahakama hii inakuachia huru kwa sharti kwamba usitende kosa lo lote la jinai kwa kipindi cha miezi 12”.

No comments:

Post a Comment