Thursday, September 17, 2015

Maonyesho ya SIDO kwa wajasiriamali kwa kanda ya kati kufanyika Agosti 26 hadi Septemba Mosi mwaka huu Mkoani Singida.

Mkuu wa mkoa wa Singida, Dk.Parseko Vicent Kone, akitoa taarifa kwa waandishi wa habari  juu  ya kufanyika kwa maonesho ya SIDO kanda ya kati kuanzia Agosti 26 hadi septemba mosi mwaka huu mjini Singida. SIDO kanda ya kati inajumuisha mikoa ya Singida, Tabora na Kigoma.Katika maonesho hayo, bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na wajasiriamali na wafanyabiashara ndogo.


Baadhi ya maafisa wa  serikali na SIDO mkoani hapa wakimsikiliza mkuu wa mkoa wa Singida, Dk.Parseko Vicent Kone, akitoa taarifa ya kufanyika maonesho ya bidhaa za wajasiriamali na wafanyabiashara ndogo kutoka mikoa ya Singida,Tabora na Kigoma. Maonesho hayo yatafanyikia kwenye viwanja vya Peoples mjini Singida.

MAONESHO ya SIDO ya jasiriamali za viwanda vidogo na biashara ndogo kanda ya kati,yanatarajiwa kufanyika katika viwanja vya Peoples mjini hapa, kuanzia agosti 26 hadi septemba mosi mwaka huu.

Hayo yamesemwa na mkuu wa mkoa wa Singida,Dk.Parseko Kone,wakati akitoa taarifa kwa wananchi kupitia vyombo vya habari juu ya kufanyika maonesho hayo mkoani hapa.

Alisema moja ya njia muhimu inayotumiwa na SIDO katika kufikisha huduma zake kwa walengwa,ni njia ya kuandaa maonesho ya bidhaa za wajasiriamali mbalimbali.

“Lengo la maonesho ya SIDO, ni kuhamasisha na kuwezesha ukuaji wa uzalishaji bidhaa na huduma katika sekta ya viwanda vidogo na vya kati,ili viweze kukuza teknolojia,kuleta tija na kuongeza ajira,kipato na hatimaye kuondoa umaskini”,alisema Dk.Kone.

Kuhusu maandalizi ya maonesho hayo, mkuu huyo wa mkoa,alisema maandalizi yote muhimu yamekamilika kwa asilimia kubwa. Maonesho hayo, huandaliwa kikanda kwa zamu kwa kushirikisha wadau wa wajasiriamali toka mikoa yote nchini.

Akifafanua,alisema kwenye maonesho hayo,pia wageni toka nchi jirani ikiwemo Kenya na Rwanda, hualikwa.

“Katika maonesho ya SIDO, mkoa wa Singida upo kanda ya kati yenye mikoa ya Tabora,Kigoma na Dodoma.Kila kanda moja inapoandaa maonesho,mikoa mingine iliyopo kwenye kanda husika,huungana na waandaji katika kuonyesha bidhaa mbalimbali za wajasiriamali wao”, alisema.

Dk.Kone alisema maonesho hayo,ni fursa kubwa kwa washiriki wote Tanzania kujifunza kwa kuona,kubadilishana uzoefu katika teknolojia,ubora wa bidhaa,taarifa za maosko na pia kuuza bidhaa zao.

Kwa mujibu wa Dk.Kone, bidhaa zitakazooneshwa ni pamoja na asali,vyakula,juize,mashine za kupura mtama,kubagua karanga,nguo aina ya batik,vikoi, bidhaa za wahunzi,bidhaa za ngozi na bidhaa mchanganyiko.


Kauli mbiu ya maonesho ya mwaka huu,ni Buni,boresha na jifunze bidhaa kupitia SIDO’.

No comments:

Post a Comment