Thursday, September 17, 2015

Taasisi za fedha ziwezeshe wajasiriamali wadogo.

Mkuu wa mkoa wa Singida, Dk.Parseko Kone, akikagua vyungu vilivyotengenezwa na wajasiriamali wa wilaya ya Iramba ambao wanashiriki maonesho ya 12 ya SIDO kanda ya kati yanayoendelea mjini Singida.
Afisa Mwanadaamizi wa Masoko wa Shirika la viwango (TBS), Gladness Kaseka (kushoto) akimpa maelezo Mkuu wa mkoa wa Singida, Dk.Parseko Kone, juu ya shughuli zinazofanywa na shirika hilo. Dk.Kone alikuwa akikagua mabanda ya wajasiriamali na taasisi mbalimbali wanaoshiriki maonesho ya bidhaa mbalimbali yaliyoandaliwa na SIDO kanda ya kati yanayoendelea mjini Singida.
Mkuu wa mkoa wa Singida, Dk.Parseko Kone, akionyesha kupendezwa na mkuki uliotengenezwa na wahunzi wa kijiji cha Kisonga wilaya ya Iramba wanaoshiriki maonesho ya SIDO kanda ya kati yanayoendelea mjini Singida.

Mkuu wa mkoa wa Singida, Dk.Parseko Kone, akionyesha kuvutiwa na bidhaa za urembo zilizotegenezwa na mjasiriamali wa kike mlemavu wa miguu, Dominion Apiyo (mwenye kofia nyeusi kulia) kutoka Kigamboni jijini Dar-es-salaam, anayeshiriki maonesho ya wajasiriamali kanda ya kati yanayoendelea Singida.
Baadhi ya vibanda vinavyotumika kwa ajili ya wajasiriamali kutoka mikoa ya Singida,Tabora, Dodoma, Kigoma na mikoa jirani wanaoshiriki kuonyesha bidhaa zao kwenye viwanja vya Peoples mjini hapa.

MKUU  wa Mkoa wa Singida, Dk Parseko Kone, amezitaka benki na taasisi za kifedha nchini, kubuni taratibu nzuri zitakazokuwa na masharti nafuu ya kukopesha, ili wajasiriamali wadogo na wa kati waweze kunufaika na mikopo hiyo itakayoongezea nguvu mitaji yao.

Amedai masharti hayo nafuu, yataondoa dhana potovu iliyojengeka kwenye  baadhi ya benki, kuwa wajasiriamali wadogo hawana sifa ya kukopesheka.

Mkuu huyo wa Mkoa, ametoa wito huo wakati akizungumza kwenye ufunguzi wa maonesho ya 12 ya kanda ya kati ya wajasiriamali wadogo na wa kati, yaliyoandaliwa na SIDO kwenye uwanja wa People’s Mjini hapa.

Pia, amezihimiza taasisi za fedha hasa benki na taasisi nyingine za kifedha, kushirikiana na SIDO katika kutoa mafunzo na ushauri wa biashara kwa wajasiriamali,ili shughuli zao ziweze kuwa na tija zaidi.

“Lengo la mafunzo yatakayotolewa  na ushauri huo, uwe dira ya kuwasaidia wajasiriamali wadogo na wale wa kati, kuandika michanganuo itakayowezesha kupata mikopo itakayoongeza nguvu katika mitaji yao.

Katika hatua nyingine, Dk. Kone alitumia fursa hiyo kusisitiza umuhimu wa wajasiriamali kuanzisha vyama vya kuweka na kukopa (SACCOS), ambavyo vitawasaidia kukopeshana wao kwa wao, kwa masharti nafuu na riba ndogo.

“Fursa hii imekuwa ikitumika pia na baadhi ya benki kukopesha wajasiriamali wadogo, ambao wapo kwenye vikundi vinavyoaminika. Lakini havina dhamana zisizohamishika za kuweka benki, ili kutimiza masharti ya kukopa”,alifafanua.

Mkuu wa mkoa huyo,ametumia fursa hiyo kuwapongeza viongozi na wananchi wa kanda ya kati, waoneshaji, uongozi na wafanyakazi wa SIDO, wafadhili na wote walioshiriki.Kwa namna moja au nyingine kufanikisha maonesho haya.

“Kwa niaba ya viongozi wa Serikali na kwa niaba yangu binafsi ninawaahidi wajasiriamali wadogo, kuwa Serikali itaendelea kuwapa Ushirikiano wa kutosha, ili kufanikisha adhima yao ya kujikwamua kiuchumi na kuongeza mapato ya Serikali.


Wakati huo huo, Dk Kone ametumia nafasi hiyo kuwahimiza wananchi wote waliojiandikisha kwenye daftari la wapiga kura, kujitokeza kwa wingi Oktoba 25 mwaka huu, kushiriki kuwapigia kura kuchagua Rais, Mbunge na Diwani atakayejali maslahi ya Taifa na wananchi wake.

No comments:

Post a Comment