Thursday, September 17, 2015

Mwanafunzi atumia bastola ya mama kutaka kujiua.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Singida, ACP Thobias Sedoyeka, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) ofisini kwake.

MWANAFUNZI wa darasa la sita katika shule ya msingi Abelt, Singida mjini Stanley Markdonard (13), amenusurika kufa katika jaribio lake la kutaka kujiuawa kwa kujipiga risasi mbili tumboni kwa kutumia bunduki aina ya bastola, mali ya mama yake mkubwa, Joyce Mark Minde.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Singida, ACP Thobias Sedoyeka, alisema tukio hilo lisilo la kawaida limetokea Agosti tatu mwaka huu majira ya mchana huko katika mtaa wa Saba Saba kata ya Mandewa manispaa ya Singida.

Alisema siku ya tukio,Stanley alivizia mama yake mkubwa akiwa kazini aliweza kuvunja mlango wa kabati na kuchukua silaha hiyo aina ya browning 7.65 MM mark No.B.097046,na kujipiga risasi mbili tumboni.

Alisema Stanley amelazwa katika hospital ya misheni ya St.Gasper Itigi wilaya ya Manyoni, na hali yake ni mbaya. Chanzo cha tukio hilo
bado linachunguzwa.

Katika tukio jingine, kamanda Sedoyeka alisema kuwa mkulima mkazi wa kijiji cha Zilingiligi kata ya Ndago wilaya ya Iramba,John Daud (45), amegongwa na basi na kufariki papo hapo.

Alisema tukio hilo limetokea Agosti mbili mwaka huu saa 1.50 usiku huko katika barabara kuu Singida – Nzenga eneo la Manguanjuki kata ya Mandewa manispaa ya Singida mjini.

“Basi lililomgonga mtembea kwa miguu John,ni T.433 BMG scania mali ya kampuni ya Mohammed trans  lililokuwa linaendeshwa na Mathias Stepheno @ Mwanamakanga (50) mkazi wa Ndala mkoani Shinyanga.Chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dreva huyo ambaye kwa sasa anashikiliwa na jeshi la polisi”,alisema.

Wakati huo huo,Sedoyeka alisema dereva wa boda boda mkazi wa Singida mjini, Khamis Salum (25),amelazwa katika hospitali ya mkoa mjini hapa,baada ya kupigwa na kitu kinachodhaniwa ni shoka na kujeruhiwa vibaya.

Kamanda huyo alisema siku ya tukio huko katika eneo la kituo cha mabasi kata ya Misuna, dereva Salum, alikodishwa na abiria ambaye hamfahamu ili ampeleke kitongoji cha Kimpungikia nje kidogo ya mji wa Singida.

“Wakiwa njiani, abiria huyo alimwambia dereva wa boda boda asimame kwa madai ameangusha simu yake ya kingajani. Dereva huyo aliposimama, ghafla abiria alimpiga kichwani na kitu kinachodhaniwa kuwa ni shoka na kisha alinyang’anywa pikipiki yake aliyokuwa anaifanyia biashara ya boda boda”alifafanua.

No comments:

Post a Comment