Sunday, October 19, 2014

Kisaki kupata maji salama.

Mhandishi wa maji manispaa ya Singida, Max Kaaya akitoa maelezo juu ya miradi ya maji kwa Naibu Waziri wa Maji Eng. Benelith Mahenge aliyekuwa ziarani mkoani Singida.

WANANCHI wa Kijiji cha Kisaki, katika Manispaa ya Singida wanatarajia kuanza kunufaika na huduma za maji safi na salama ifikapo mwishoni mwa mwezi ujao, baada ya mradi wa maji unaotarajiwa kutumia zaidi ya shilingi milioni 55.1 utakapokamilika.

Mhandisi wa maji wa Manispaa ya Singida,Injinia Max Kaaya alifafanua kwamba mradi huo ulioanza kutekelezwa kuanzia mwezi, julai mwaka jana unatarajiwa kukamilika kujengwa mwishoni mwa mwezi ujao.

Kwa mujibu wa Injinia huyo kati ya kiasi hicho cha fedha, nguvu kazi za wananchi zinatarajiwa kuokoa zaidi ya shilingi
milioni mbili na kwamba kiasi cha fedha kilichosalia zimetolewa na serikali kuu chini ya mradi wa maji na usafi wa mazingira, maarufu kwa jina la mradi wa Benki ya Dunia.

Hata hivyo Injinia Kaaya alisema mradi huo utakapokamilika unatarajia kuwanufaisha wakazi 3,977 wa Kijiji cha Kisaki kwa kupata huduma za maji hayo safi kwenye vituo vya kuchotea maji (DPs ) 25 .

Injinia Kaaya hata hivyo alifafanua pia kwamba hadi sasa mradi huo umekamilika kwa asilimia 74 na kuzitaja kazi zilizokamilika kuwa ni pamoja na ujenzi wa tenki,vituo 10 (DPs) vya kuchotea maji,ulazaji wa bomba zenye urefu wa kilometa 14 na ujenzi wa kibanda cha mashine ya kusukuma maji.


Halmashauri ya Manispaa ya Singida inatarajia mradi huo utakamilika katika muda uliopangwa,na kwamba unatarajiwa pia kupunguza tatizo la uhaba wa maji safi na salama,ikiwa ni pamoja na kupunguza umbali wa kufuata maji usiozidi mita 400.

No comments:

Post a Comment