Sunday, October 23, 2011
Gaddafi ana utajiri wa Sh 140 trilioni:NI SAWA NA BAJETI YA TANZANIA KWA MIAKA 12
KIONGOZI wa Libya aliyeuawa juzi na wapiganaji wa Serikali ya Mpito (NTC), anadaiwa kuacha utajiri wa Sh 139 trioni kiasi ambacho ni sawa na bajeti ya Tanzania kwa miaka 12. Habari zilizopatikana jana zimeeleza kuwa fedha hizo ni zile zinazofahamika, alizoweka kwenye benki za nchi kadhaa duniani, huenda alikuwa na hazina zaidi mbali na hiyo.
Kwa mujibu wa habari hizo, Gaddafi alikuwa anamiliki Pauni 29 bilioni nchini Uingereza (Sh78 trilioni), Dola 32 bilioni nchini Marekani (Sh54 trilioni) , Dola 2.4 bilioni nchini Canada( Sh4 trilioni) na Dola 1.7 bilioni nchini Australia (Sh3 trilioni). Kwa fedha ya Tanzania. Pauni moja ya Uingereza ni sawa na Sh 2,720, Dola moja ya Marekani Sh 1,704, Dola moja ya Canada, Sh 1,692 na Dola ya Australia ni Sh 1,769.
Fedha hiyo kwa ujumla wake ni sawa na bajeti ya Tanzania kwa miaka 12. Juni mwaka huu, Bunge lilipitisha jumla ya Sh11 trilioni kwa matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2011/2012 .Kiasi hicho kikizidishwa mara miaka 12 zitakuwa Sh132 trilioni, hivyo ukichukulia kiwango hicho, inamaana kuwa fedha za Gaddafi zinatosha kuendesha Tanzania kwa miaka 12 na bado zitabaki Sh trilioni saba.
Alikuwa na nywele, sura bandia
Vipimo vya DNA vilivyofanywa kwenye mwili wa Gaddafi, vimebaini kuwa kiongozi huyo wa zamani wa Libya, alikuwa na nywele bandia, Jarida la Washington Post limeripoti.Waziri Mkuu wa muda wa Libya, Mahmoud Jibril aliliambia jarida hilo kuwa wachunguzi walifanya vipimo vya damu, mate na nywele na kugundua kuwa nywele hizo si halisi.
Mwili wa kiongozi huyo kwa sasa umehifadhiwa ndani ya msikiti mmoja nje ya mji wa Sirte alikokamatwa na kuuawa ukisubiri kuzikwa baada ya uchunguzi unaotarajiwa kufanywa na Umoja wa Mataifa.
Mwaka 1995, Gaddafi aliwahi kufanyiwa upasuaji wa uso kwa kile alichodai kuwa hataki kuonekana mzee.
“Aliniambia kuwa amekaa madarakani kwa miaka 25 wakati huo na kwamba hataki vijana wa taifa lake wamwone mzee,” alisema Dk Liacyr Ribeiro kutoka Brazil aliyemfanyia upasuaji huo.
Kwa mujibu wa Washington Post, Gaddafi aliwekewa nywele bandia pia aliwekewa mafuta kwenye uso wake yaliyotolewa tumboni, ili kupunguza uwezekano wa uso wake kuonekana wa kizee.
Familia yaomba mwili wa Gaddafi
Mke wa Kanali Gaddafi, Safia, ameibuka na kutaka apewe mwili wa mumewe ili ukazikwe na familia kisha Umoja wa Mataifa ufanye uchunguzi wa kina juu ya kifo chake.Akizungumza kupitia Televisheni ya Rai Tre ya Italia, akiwa uhamishoni nchini Algeria, Safia alisema ni muhimu uchunguzi wa kifo hicho ufanyike ili kujua kama haki ilitendeka ama la.
"Hayo ni makubaliano na familia yangu kwamba tunaomba ufanyike uchunguzi wa kina na baada ya kumalizika kwa uchunguzi tuletewe mwili wake, tutazika wenyewe,"alisema Safia.
Mazishi ya Gaddafi yanayoelezwa kutaka kufanywa kwa siri, yamesitishwa kutokana na tofauti zilizoibuka miongoni mwa maofisa wa Libya baada ya baadhi kutaka ahifadhiwe na wengine atupwe baharini.
Safia alisema; "Kwa utamaduni wa Kiislamu, maziko ya Gaddafi yanapaswa kufanyika haraka iwezekanavyo na sio kuhifadhiwa kwa siku kadhaa. Naomba uchunguzi ufanyike tena wa kimataifa ili ibainike chanzo cha kifo cha Gaddafi," alisema Safia ambaye alieleza kuwa wanawe, walipiga simu ya baba yao mara baada ya kusikia amefariki dunia, lakini mara zote simu hiyo ilipokelewa na waasi.
Kwa mujibu wa vituo vya televisheni vya Dubai na Jordan juzi, mtoto wa kike wa Gaddafi Ayesha, akizungumza kutoka Algeria, alilalamika kwamba waasi wamemuua baba yake na kumfanyia ukatili mkubwa.
"Niliposikia baba yangu ameuawa sikuamini nikampigia simu lakini, ikapokelewa na mapanya hao (waasi) wa Mediteranian," alisema. Ayesha aliungana na mama yake Safia kutaka wapewe mwili wa baba yao ili wakamzike wenyewe, badala ya kuzikwa na waasi hao alioeleza kuwa hawana haki tena dhidi yake, baada ya kumwua.
Ameutaka Umoja wa Mataifa (UN) usaidie urejeshwaji wa mwili wa Gaddafi kwa familia yake ili ndugu na jamaa wamwage na kumzika kwa heshima zote.Hata hivyo, Kamishna wa Kutetea Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Navi Pillay, alisema ni lazima uchunguzi wa kina ufanyike dhidi ya kifo hicho.
Kaimu Waziri Mkuu wa Libya, Jibril alisema kwamba Kanali Gaddafi alipigwa risasi kichwani wakati alipojaribu kurushiana risasi na waasi.
Serikali mpya kutangazwa leo
Baada ya kifo cha Gaddafi, Serikali mpya ya nchi hiyo inatarajiwa kutangazwa leo. Msemaji wa Jeshi la Libya Abdel-Rahman Busin, alisema kwamba watatangaza kuzaliwa upya kwa Serikali yao katika mji wa Benghazi.
Alisema Serikali hiyo mpya inaiomba familia ya Gaddafi kuhudhuria sherehe hizo za utambulisho Serikali mpya bila wasiwasi wowote kwani baada ya mapinduzi hayo, Libya sasa ni nchi ya kidemokrasia.
“Leo (jana) watu wana furaha na furaha hiyo itaongezeka zaidi kesho (leo) baada ya kutangazwa kwa Serikali yetu mpya ambayo itakuwa ya wananchi wote bila ya ubaguzi,”alisema. Msemaji huyo wa jeshi alieleza kuwa mazishi ya Gaddafi bado hayajajulikana yatafanyika lini lakini kwa vyovyote vile yatasubiri uchunguzi unaotarajiwa kufanywa na Umoja wa Mataifa (UN) wakati wowote kuanzia sasa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment