VURUGU, milio ya risasi za moto na mabomu ya machozi jana ziligubika mji wa Dodoma kufuatia wakazi wa Mtaa wa Njedengwa, Kata ya Dodoma Makulu kupambana na polisi kupinga hatua ya Manispaa ya Dodoma kuvunja nyumba zao.
Vurugu hizo zilizoanza saa 11.30 alfajiri zilisababisha watu 12 kujeruhiwa vibaya baada ya polisi kutumia mabomu ya machozi na risasi za moto kukabiliana na wakazi wa mtaa huo maarufu mjini Dodoma, wanaodaiwa kuvamia na kujenga katika eneo la mwekezaji.
Risasi za moto zilianza kusikika eneo la tukio huku kundi la polisi pamoja na vijana wenye nguvu (mabaunsa) wakiwa wametanda eneo hilo na kufanya ligeuke uwanja wa mapambano.Mabaunsa hao ambao walikuwa wamefunika nyuso na kuacha sehemu ya macho, waliingia kila nyumba na kuwashambulia waliokuwa ndani huku huku wakiwalazimisha kutoka nje.
Hata hivyo, licha ya polisi kuwa na silaha za moto, wenyeji hao hawakukubali kutii amri, walitoka na silaha za jadi mishale, mapanga na mawe ili kupambana kuzuia bomoa bomoa hiyo.
Baadhi yao walirusha mishale na wengine kutumia mapanga kujihami kila walipovamiwa na vijana hao wenye miraba minne . Hata hivyo wenyeji hao kutokana na silaha dhaifu, walizidiwa nguvu na kujikuta wengi wao wakiwekwa chini ya ulinzi.
Wakati wanaume wakipambana na askari hao, vilio vya akina mama na watoto vilisikika kutoka kila upande huku mabomu ya machozi yaliyokuwa yakipigwa mfululizo yakizidi kuwachaganya.
Hatua ya kubomoa nyumba hizo ilitokana na hukumu ya Mahakama iliyompa haki mtu anayefahamika kwa jina la Maimu (Sinana Enterprises ) kuwa ni mmiliki halali wa eneo hilo ambalo amepewa na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kwa ajili ya kujenga shule.
Kwa mujibu wa maelezo kutoka kwa wenyeji wa eneo hilo, mwekezaji huyo wakati anapewa sehemu hiyo, tayari kulikuwa na nyumba za watu waliokuwa wakiishi hapo kwa muda mrefu.
“Kwa mfano mimi hapa, nilikuta kuna msitu mwaka 1987 nikaanza kulima na mwaka uliofuata nilijenga hii nyumba yangu, lakini huyo mwekezaji yeye alikuja mwaka 2004 sasa jamani kuna haki hapo?’’Alisema mama mmoja ambaye jina lake halikupatikana baada ya kutishiwa kukamatwa na askari aliyekuwa jirani na kumtaka aondoke ili tingatinga libomoe nyumba yake.
Eneo la tukio
Kwa kiasi kikubwa mabaunsa hao wa kampuni iliyopewa kazi na mwekezaji kusimamia ubomoaji huo, ndio walioonekana kuchochea moto huo zaidi, kwani kila wakati walisikika wakitoa lugha za vitisho kwa wenyeji huku wakiwa wamevalia kofia za kufunika uso.“Habaki bweha hapa, lazima mfundishwe adabu zenu maana sisi tumekuja kikazi zaidi na hamtatusahau kabisa maishani mwenu,’’ alisika mmoja wao akisema.
Mali zaharibiwa
Nyumba nyingi zilizobomolewa zilikuwa na vitu mbalimbali vya thamani, isipokuwa wale waliowahi kutoa vyombo vyao nje ambapo tingatinga hilo la CDA halikuweza kuvigusa.
Baadhi ya maduka yalivunjwa na bidhaa zikiwa ndani huku vijana waliokuwepo aneo hilo, wakisomba bia na kugawana baadhi ya vitu hali iliyolazimisha polisi kuanza kuwazuia.
CDA wakataa kubebeshwa lawama
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA), Martin Kitila alikanusha vikali kuhusika kwa mamlaka yake kwenye bomoa bomoa hiyo kwa maelezo kwamba anayevunja, ni mwenye eneo hilo.
“Sisi hatuhusiki kabisa katika uvunjaji huo maana tulishamlikisha mhusika, yeye ndiye mwenye mamlaka ya kufanya atakavyo,’’ alisema Kitila.
Alipotakiwa kueleza ni kwa nini vyombo vyake vimehusika Mkurugenzi huyo alisema, “Hilo sio tatizo kwani mtu yeyote anaweza kuja kuazima vifaa kwetu na tukifikia makubaliano, sisi tunampa’’.
Hata hivyo, Mkurugenzi huyo alipinga suala na wananchi kupewa namba na CDA kuwa ni kigezo cha kuhalalishwa na badala yake alisema namba zinazobandikwa huwa ni kwa ajili ya kuwatambua tu wakazi hao, lakini si uhalali wa kuishi au kupimiwa viwanja.
Vyombo vya habari
Vurugu hizo pia zilizua balaa kwa waandishi wa habari waliokuwa kazini eneo ambao walijikuta wakishambuliwa na polisi waliokuwa wakiwakataza kufanya kazi.
Waandishi wa Mwananchi, walijikuta pikipiki yao ikivunjwa kioo na polisi aliyewalalamikia kuwa gazeti lao ni wambeya huku akiwataka wakaandike chochote watakacho. Polisi pia walikuwa wakizuia waandishi kupiga picha.
Licha ya kuonyesha vitambulisho vyao, mwandishi Masoud Masasi na mfanyakazi mwenzake wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd, Ali Jumanne waliofika eneo la tukio kwa pikipiki, walipigwa na kuzuiliwa kwa muda hadi mmoja wa waandishi alipofika na kuwasaidia ingawa baadaye askari hao waliomba radhi.
Katika vurugu hizo Jumanne alijeruhiwa mguu wa kushoto.
Kwa upande wao Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), gari yao ilivunjwa vioo na wananchi kwa madai kuwa hawataki kuwaona kwani ni watu wa Serikali, kabla ya mtangazaji wa Radio Mwangaza, Jane Charles kushambuliwa kwa mawe na wananchi hao na kujeruhiwa.
Kamanda wa Polisi
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Zelothe Stephen hakuweza kuzungumzia tukio hilo kwani muda wote simu yake ilikuwa ikipokelewa na mtu aliyejitaja kwa jina la Yohana na kujitambulisha kuwa ni msaidizi wake.“Mimi ni msaidizi wa Kamanda naitwa Yohana, muda huu Kamanda hawezi kuzungumza na ninyi, yuko kwenye mapokezi ya Mwenge mtafute baadaye,’’alisema mtu huyo na kukata simu.
Mwenye Kampuni
Msemaji wa Kampuni la Sinana ambaye alijitambulisha kwa jina la Mujibu Ali, alisema kuwa kampuni hiyo ilipewa hati ya kumiliki eneo hilo tangu mwaka 2004 na kwamba hapakuwa na nyumba katika eneo lote.
“Hapa tunamiliki ekari 21 ambazo tunataka kujenga shule na tulianza kumiliki tangu mwaka 2004, lakini hawa jamaa walikataa kuondoka na kesi tulishinda mahakamani tangu Julai 25 mwaka huu na kuwapa notisi, lakini bado hawakuondoka,’’alisisitiza Ali.Majeruhi.Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Dk Nassoro Mzee alisema walipokea majeruhi 12 na kukanusha kutokea kwa kifo kwenye tukio hilo.
“Ni kweli tumepokea majeruhi 12 hapa, lakini waliolazwa hadi sasa ni tisa, kati yao wanawake wawili na wanaume ni saba." Wagonjwa hao wanaonekana wamejeruhiwa katika maeneo mbalimbali ya miili yao hata hivyo siwezi kuthibitisha kama ni risasi maana hadi tuzitoe mwilini,’’alisema Mzee.
Akizungumza kwa tabu katika wodi namba moja mmoja wa majeruhi hao aliyejitambulisha kwa jina la Mukoro Maro, alisema alikatwa mapanga na mabaunsa wakati akijaribu kukoa familia yake.
“Polisi walinikamata na kunipeleka kwa vijana waliovaa kofia za kuficha nyuso ambao walinishambulia kwa mapanga na kunipora simu yangu, alisema Maro huku akiwa amelowa damu kutokana na majeraha makubwa kichwani.
Kwa upande wake Yohana Charles, alisema kuwa yeye alistukia kitu cha moto katika paja la mguu wake wa kushoto wakati akienda kumsaidia mzee aliyekuwa anapigwa na polisi ghafla alianguka chini na kupoteza fahamu baadaye alijikuta hospitalini na kugundua kuwa amepigwa risasi.
Ulinzi hospitalini
Eneo la Hospitali ya Mkoa wa Dodoma lilikuwa na ulinzi mkali, polisi wakiwa wametanda kila kona na silaha za moto hali iliyowatisha watu wengi waliokuwa wakienda hapo kusalimia wagonjwa wao.
JAMANI HUYU SINANA ENTERPRISES NI HATARI ANADHULUMU WATU SANA NA ANAJIMILIKISHA MAENEO KIBABE SANA NA ANAONEA SANA WATU NA ANATUMIA PESA KUHONGA NA KUDHULUMU WATU SASA HIVI FUATILIENI TENA MTAKUTA ANA KESI YA KUTAPELI SHULE HUKO IPAGALA
ReplyDelete