Tuesday, November 25, 2014

Singida wajipanga kufanikisha uchaguzi wa serikali za mitaa.

Mkurugenzi wa manispaa ya Singida, Joseph Mchina, akitangaza ratiba ya uchaguzi wa serikali za mitaa kwa mwaka huu,mbele ya waandishi wa habari.
Baadhi ya waandishi wa habari mjini Singida, wakimsikiliza mkurugenzi wa manispaa ya Singida, Joseph Mchina (hayupo pichani) wakati akitangaza ratiba ya uchaguzi wa serikali za mitaa ulioanza Novemba 16 mwaka huu.

Round about ya manispaa ya Singida iliyopo barabara kuu ya Singida-Mwanza eneo la Peoples klabu.

HALMASHAURI  ya manispaa ya Singida,imejipanga vema kwa ajili ya kuhakikisha uchaguzi wa serikali za mitaa 2014, unakuwa huru,haki  na wa amani.

Hayo yamesemwa na msimamizi wa uchaguzi wa manispaa hiyo, Joseph Mchina, wakati akitangaza ratiba ya uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu mbele ya waandishi wa habari.

Mchina ambaye ni Mkurugenzi wa manispaa ya Singida,alisema nafasi zitakazogombewa ni pamoja na uenyekiti wa mtaa/kijiji,ujumbe wa kamati ya mtaa, ujumbe wa halmashauri ya kijiji na uenyekiti wa kitongoji.

Alisema fomu zilianza kuchukuliwa na kurejeshwa  juzi (16/11/2014) na mwisho wa zoezi hilo ni novemba 23 mwaka huu saa 10.00 jioni.


“Fomu zitaanza kuchukuliwa kuanzia saa mbili asubuhi mpaka saa 10.00 jioni kutoka
ofisi ya msimamizi msaidizi wa uchaguzi ambao ni za WEO,MEO na VEO”,alifafanua Mchina.

Aidha,alisema kuwa uteuzi wa wagombea utafanyika novemba 24 mwaka huu na baada ya uteuzi,msimamizi msaidizi wa uchaguzi,atabandika majina ya wagombea wenye sifa na wasio na sifa za kugombea nafasi hizo.

Akifafanua zaidi kuhusu kujipanga huko, Mchina alisema kuwa wametoa matangazo ya kutosha yanayotoa ufafanuzi wa sheria,kanuni na taratibu zinazotawala uchaguzi huo.

“Tumefanya semina za kutosha kwa watendaji  na waandikishaji wa uchaguzi huu.Vile vile tumekaa na vyama vyote vya siasa vilivyopo kwenye manispaa yetu na tumekubaliana kuwepo na nidhamu ya hali ya juu wakati wote wa uchaguzi huu”,alisema.


Katika hatua nyingine,msimamizi huyo ametahadharisha kwamba mtu atakaye fanya makosa ya uchaguzi kwa mujibu wa kanuni 34 ya uchaguzi huu,atafikishwa mahakamani na endapo atapatikana na hatia,atatozwa faini isiyozidi shilingi 50,000 au kifungo cha miezi 12 au vyote kwa pamoja.

Wakati huo huo,msimamizi huyo ametoa wito kwa wakazi wa manispaa ya Singida wenye umri kuanzia miaka 21 na kuendelea wenye sifa za uongozi,wajitokeze kwa wingi kuomba nafasi za uongozi zilizotangazwa.

“Naomba nitumie nafasi hii niwaombe wananchi wote wenye sifa za kujiandikisha kupiga kura kwa maana awe na umri kuanzia miaka 18 na kuendelea.Awe Mtanzania na mkazi wa kawaida katika kitongoji,kijiji au mtaa,ajitokeze kujiandikisha kupiga kura.

Pia wajitokeze kusikiliza kampeni za wagombea na siku ya uchaguzi wajitokeze kwa wingi kupiga kura kuchagua viongozi wanaowataka”,alisema Mchina.


Halmashauri ya manispaa ya Singida,inatarajiwa kuwa na vituo 160 za kupigia kura na inatarajiwa kutumia zaidi ya shilingi 25 milioni kugharamia uchaguzi huo.

No comments:

Post a Comment