Jeraha la Mwanamke (30) aliyeunguzwa pasi ya umeme na mumewe mjini Singida.
Jeshi
la polisi Mkoani Singida linamshikilia mtu mmoja Baltazar Mushi
Sammayuni (33), kwa tuhuma ya kumuunguza mkewe usoni, kwa kutumia pasi
ya umeme wakati akiwa amelala usiku wa manane nyumbani kwao.
Kaimu
kamanda wa polisi mkoani Singida Thobias Sedoyeka amesema tukio hilo la
kusikitisha lilitokea siku ya
ijumaa iliyopita saa kumi alfajiri
nyumbani kwao katika eneo la Ipembe mjini Singida.
Amesema
kuwa, Sammayuni anayejishughulisha na biashara, alifunguliwa mlango
usiku, lakini kutokana na sababu ambazo bado zinachunguzwa aliiwasha
pasi ya umeme wakati mkewe akiwa kwenye usingizi mzito na kumuunguza
usoni sehemu ya shavu la kushoto.
Amesema
kuwa mwanamke huyo amejeruhiwa vibaya lakini baada ya kupatiwa tiba
katika hospitali ya mkoa wa Singida aliruhusiwa na hali yake inaendelea
vema.
Sedoyeka amesema kuwa wanatarajia kumfikisha mtuhumiwa mahakamani wakati wowote baada ya upelelezi kukamilika.
Kutokana
na tukio hilo, Sedoyeka ametoa wito kwa wanandoa kuacha kujichukulia
sheria mkononi kwa kuwa kila mtu anayo haki ya kuishi na yeyote
atakayekiuka, mkono wa sheria utafanya kazi yake.
Aidha
mwanamke huyo (30) akizungumza na Singida Yetu Blog nyumbani kwake mjini Singida
kwa sharti la kutotajwa jina, amesema baada ya mumewe kufika usiku na
kumfungulia mlango, yeye alilala lakini alishitushwa na maumivu makali
usoni hali iliyomlazimu kuamka ghafla.
Amesema
alikimbilia kwenye kioo kikubwa na alipojitazama aligundua uso wake
sehemu ya shavu la kulia ameunguzwa na pasi na alipomuuliza mumewe
sababu ya kuchukua uamuzi huo alijibiwa kuwa ameamua tu kufanya hivyo.
“Kwa
kweli roho inaniuma sana, nilipomuuliza akanijibu ameamua tu kufanya
hivyo?…kesho yake akanieleza kumbe hata jicho sikutoboa”, nilitakiwa na
hayo macho yote niyatoboe kabisa ili usiendelee kuona tena,”alisema
mwanamke huyo jinsi mumewe alivyomkejeli.
Sedoyoka
ambaye ni mkuu wa upelelezi makosa ya jinai amesema mtuhumiwa
atafikishwa mahakamani wakati wowote wiki hii kujibu shitaka lake.
No comments:
Post a Comment