Waziri wa Mali asili na Utaliii na Mbunge wa jimbo la Singida kaskazini,Lazaro Nyalandu.
KANISA jipya la Miracle Assemblies of God Ministry (MAGM) mkoani Singida linatarajia kutumia zaidi ya shilingi 214.1 milioni kugharamia ujenzi wa shule ya awali ya bweni.
Hayo yalisemwa hivi karibuni na Magreth Ndwete wakati akisoma risala fupi ya kanisa hilo kwenye hafla ya kusimikwa kwa askofu wa kwanza wa kanisa hilo John Sanongo Tesha (58), Mgeni rasmi katika hafla hiyo,alikuwa Waziri wa Mali asili na Utaliii na Mbunge wa jimbo la Singida kaskazini,Lazaro Nyalandu.
Amesema shule hiyo ambayo tayari imeisha anza kwa kuwa na vyumba viwili vya madarasa itachukua wanafunzi wa madhehebu yote ya dini na wale ambao hawana dini kama watakuwepo.
Amesema kanisa hilo lililoanza rasmi juni 11 mwaka 2007 na kupata usajili novemba 21 mwaka jana,pamoja na kutoa huduma ya kiroho pia limeamua kutoa huduma ya kijamii kwa kuanzisha shule ya awali.
“Kwa kuanzia waumini wa kanisa hilo waliamua kuchangishana wao kwa wao na kufanikiwa kupata zaidi ya shilingi
17.8 milioni ambazo zimegharamia ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa ambavyo hivi sasa vinatumika”amesema Ndwete.
Aidha, amesema kwa kuanzia wanatarajia kuanza na wanafunzi 80 na lengo ni kuongeza wanafunzi kadri Mungu atakavyowawezesha kuwa na uwezo wa kuongeza vyumba vya madarasa na mabweni.
“Uongozi wa kanisa la Miracle unatoa shukrani kwa waumini wake wote waliojitolea kwa hali na mali,kuhakikisha kuwa kanisa hilo limefikia hatu hii nzuri tunayoiona”,amesema.
Wakati huo huo,mgeni rasmi Waziri Nyalandu ameahidi kulichangia kanisa hilo zaidi ya shilingi 75 milioni,ili liweze kupiga hatua katika ustawi wake.
No comments:
Post a Comment