Friday, April 18, 2014

Waandishi wa habari Singida wapata mafunzo ya haki za binadamu.

Mwezeshaji wa mafunzo, Lilian Timbuka, akitoa mada yake kwenye mafunzo yanayohudhuriwa na waandishi wa habari mkoa wa Singida,yanayohusu maadili katika uandishi wa habari na kuripoti masuala yaliyo kwenye mazingira magumu.
Mwezeshaji Lilian Timbuka,akitoa mada yake wakati akifundisha waandishi wa habari mkoa wa Singida, juu ya maadili ya uandishi wa habari na kuripoti masuala yanayojitokeza kwenye mazingira magumu.Mafunzo hayo ya siku nne,yameandaliwa na kufadhiliwa na Baraza la habari Tanzania (MCT).
Mmoja wa waandishi wa habari katika mafunzo,Alice Achieng Obwanoa,akiwasilisha majumuisho ya kazi waliyopewa kuifanya katika kikundi chao ikiwa ni sehemu ya mafunzo ya maadili ya uandishi wa habari na masuala ya kuripoti habari za mazingira magumu.
Baadhi ya waandishi wa habari mkoa wa Singida, wanaohudhuria mafunzo ya siku nne yanayohusu maadili katika uandishi wa habari na kuripoti masuala yanayojitokeza kwenye mazingira magumu.

JUMLA ya waandishi wa habari 23 kutoka vyombo mbalimbali vya habari mkoani hapa wanahudhuria mafunzo yanayolenga kuwaongezea uwezo zaidi wa kuzingatia maadili ya uandishi wa habari na kuripoti kwa ufasaha masuala yaliyo kwenye mazingira magumu.

Mafunzo hayo ya siku nne,yameandaliwa na kufadhiliwa na Baraza la habari Tanzania (MCT) yanaendelea kwenye ukumbi wa mikutano wa Singida Press Club mjini hapa.

Baadhi ya mada zitakazotolewa au kufundishwa ni pamoja na haki za binadamu,haki za binadamu kimataifa,machafuko yanaanzaje,masuala ya usalama kwa mwandishi na wajibu wa wahariri wa habari.

Kwa upande wake Mwezeshaji wa Mafunzo hayo,Lilian Timbuka amewataka waandishi wa habari kufanya kazi kwa kujitambua na kwa weledi wa hali ya juu.

“Mwandishi wa habari kwa kutumia kalamu yako unaweza ukaijenga nchi yako kwa kipindi kirefu.Lakini pia kwa kutumia kalamu hiyo hiyo unaweza
kuibomoa nchi yako kwa sekunde chache sana”,amesema.

Kwa hali hiyo,amesema mwandishi wa habari akijitambua na akazingatia maadili ya uandishi wa habari,wakati wote atakuwa kwenye upande wa kuijenga nchi yake na sio kuibomoa.

Aidha,Lilian amewataka waandishi wa habari kujitahidi kujiepusha na vitendo ambavyo vitaifanya tasnia ya habari kuwa jalala na kupelekea isiaminike kabisa mbele ya macho ya jamii.

“Tasnia yetu ni lazima tuilinde iendelee kuaminika na jamii wakati wote ili pamoja na mambo mengine tukiielimisha jamii juu ya kuacha kutenda maovu itatuamini na hivyo kuacha kutenda maovu ya aina mbalimbali ambayo kwa kiwango kikubwa hubomoa”,amesema.

Mwezeshaji huyo, amewataka kujiepusha na uandishi wa mashinikizo,ushabiki,upendeleo,za kubeba viongozi na badala yake waandiki habari za ukweli,zinazozingatia haki kwa pande zote mbili (balance).


“Hakikisheni wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yenu,mnazingatia haki za binadamu.Stori zenu zisiwe na upendeleo kabisa,unyanyasaji,stori zenu zizingatie maadili ya uandishi wa habari wakati wote”,alifafanua Lilian.

No comments:

Post a Comment