Saturday, April 26, 2014

Wajasirimali washauriwa kushiriki maonyesho yanayoandaliwa na SIDO.

Mkuu wa wilaya ya Singida, Queen Mlozi akizungumza wakati wa kufungua mafunzo ya usindikaji nyanya,biashara na masoko yaliyohudhuriwa na wajasiriamali 36 kutoka Manispaa na Wilaya ya Singida.Kulia ni meneja wa SIDO mkoa wa Singida, Shoma Kibende.

WAJASIRIAMALI Wilayani Singida wamehimizwa kujenga utamaduni wa kushiriki maonesho ya kanda ya kati yanayosimamiwa na SIDO ili pamoja na mambo mengine kutangaza bidhaa zao ziweze kupata soko la uhakika na linalolipa vizuri.

Wito huo umetolewa hivi karibuni na Mkuu wa Wilaya hiyo, Queen Mwashinga Mlozi wakati akifungua mafunzo ya usindikaji nyanya,biashara na masoko yaliyohudhuriwa na wajasiriamali 36 kutoka Manispaa na Wilaya ya Singida.

Amesema ili waweze kupata soko la uhakika na lenye manufaa wanapaswa kuhakikisha bidhaa zao zinakuwa na ubora unaokidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi.

“Pia muelewe kuwa biashara yo yote inahitaji uelewa wa soko.Naamini mafunzo ya biashara na masoko mliyopata yatawawezesha kuwa na uelewa mzuri wa soko”amesema Mlozi na kuongeza;

“Nachukua nafasi hii kuwahimiza kuwa soko ni
kwa bidhaa zenye ubora,kujitangaza na kufungasha kwa vifaa vinavyokubalika na vyenye ubora”.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amesema anafahamu kuwa soko la bidhaa za matunda na mbogamboga ni gumu hivyo amewataka kujituma zaidi na kutumia ujuzi wanaoupata kupitia mafunzo ili waweze kupunguza kiwango kinachoharibika.


Wakati huo huo, Mlozi ametumia fursa hiyo kuyapongeza mashirika yasiyo ya kiserikali ya SIDO na HELVETAS kwa ushirikiano wao katika jitihada za kukuza uchumi kwa wajasiriamali wa wilaya ya Singida.

No comments:

Post a Comment