Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dk. Shukuru Kawambwa.
JUMLA ya wanafunzi 2,006 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu mkoani hapa bado hawajaripoti katika shule walizopangiwa.
Hayo yamesemwa hivi karibuni na Afisa Kazi Sekretariati mkoani Singida,Jacob Elias wakati akitoa taarifa ya usajili wa wanafunzi kidato cha kwanza mwaka huu mbele ya kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilichofanyika katika ukumbi wa mkutano wa Chuo cha Mafunzo na Ufundi Stadi (VETA) mjini Singida.
Amesema wanafunzi hao ambao bado hawajaripoti hadi sasa ni sawa na asilimia 19 ya wanafunzi wote 10,802 waliofaulu mtihani wa taifa wa kumaliza shule za msingi.
Akifafanua,Jacob amesema wilaya ya Manyoni inaongoza kwa wanafunzi 585 ambao hawajaripoti kuanza kidato cha kwanza hadi sasa.
“Manyoni inafuatiwa na Wilaya ya Ikungi ambayo wanafunzi 503 hawajaripoti kuanza kidato cha kwanza hadi sasa.Iramba 318, Manispaa ya Singida 270, Singida vijijini 238 na Mkalama 92″, amesema Jacob.
Amesema kila Halmashauri na Manispaa zinapaswa kuweka mikakati bora na sahihi ili kuhakikisha kila mwanafunzi aliyefaulu, ajulikane yupo wapi aweze kufuatiliwa na kuanza masomo.
Kuhusu ajira ya walimu wapya,Jacob amesema mkoa umepangiwa walimu wapya
469 nwa shule za msingi na 636 wa shule za sekondari.
“Kwa upande wa walimu hao wapya wa sekondari,sanaa imepangiwa walimu 129 wenye diploma na 418 wenye digrii.Sayansi wenye diploma ni 36 na digrii 53″,amesema.
Jacob amesema kutokana na mchanganuo huo, walimu wa sayansi na hisabati ni 89 na hili bado ni janga kubwa kwa mkoa wa Singida na taifa kwa ujumla.
Amesema walimu hao wachache,watumiwe kikamilifu ili waweze kuzalisha wanasayansi wengi watakaopelekea kupata walimu wa kutosha wa sayansi kimkoa na kitaifa kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment