Friday, April 11, 2014

Serikali, wananchi wahimizwa kuendeleza miradi iliyoanzishwa na wahisani.


Mratibu wa mradi wa ushiriki sawa wa wanaume katika masuala ya afya ya uzazi na ujinsia (TMEP) mkoa wa Singida, Mary Sirima, akitoa taarifa yake ya utekelezaji wa mradi huo kwa waandishi wa habari (hawapo kwenye picha)
Baadhi ya wataribu wa mradi wa ushiriki sawa wa wanaume katika masuala ya afya ya uzazi na ujinsia (TMEP) waliohudhuria semina ya siku moja ambayo ilihusu kuwajengea uwezo zaidi wa kutoa elimu kwa jamii.
SERIKALI na Asasi zake zimeshauriwa kujenga utamaduni wa kuendeleza miradi ya maendeleo inayoanzishwa na wahisani wa maendeleo ili pamoja na mambo mengine kuifanya miradi hiy ya wananchi kuwa endelevu.

Imedaiwa miradi mingi ya maendeleo ya wananchi inayoanzishwa na wahisani wa maendeleo kufa baada ya kukabidhiwa wananchi na serikali,

Wito huo umetolewa mwishoni mwa wiki na Mratibu wa Mradi wa ushiriki sawa wa wanaume katika masuala ya afya ya uzazi na jinsia (TMEP) Mkoa wa Singida,Mary Sirima wakati akitoa taarifa yake ya maendeleo ya mradi huo ulioanza mwaka 2010/2011 ambao umepangwa kukamilika desemba mwaka huu.

Amesema miradi karibu yote inayoanzishwa na wahisani wa maendeleo lengo kuu huwa ni kuisaidia serikali katika juhudi zake za kuwaondolea wananchi kero mbalimbali zinazowakabili.

Akifafanua zaidi, Sirima amesema pamoja na kuwaondolea kero wananchi ipo miradi mingi tu ambayo inakuwa chachu ya maendeleo katika sehemu husika.

“Kutokana na ukweli huo upo umuhimu mkubwa kwa serikali na taasisi mbalimbali na hata watu wenye uchumi mzuri kuchukua hatua ya kuendeleza miradi inayoanzishwa na wahisani ili iwe endelevu “,amesema Mratibu huyo.

Kuhusu TMEP, Sirima amesema kuanzishwa kwa mradi huo katika
kata 62 za wilaya ya Singida vijijini na Manyoni wamewafikia watu zaidi ya milioni moja na kuwapatia elimu ya afya ya uzazi na jinsia.

Amesema lengo hilo limejikita zaidi kwa upande wa wanaume na msisitizo kwao ni kwamba wawe chachu ya mabadiliko katika masuala ya afya ya uzazi na ujinsia.

“Lengo letu au matarajio yetu ni kwamba tunataka wanaume wajenge utamaduni wa kuwasindikiza wake zao kliniki na wasione aibu kuwasaidia kufua nguo za watoto wakiwemo wachanga kupika na kufanya kazi zote za nyumbani, amedai hatua hii pamoja na faida zake nyingi itaimarisha upendo ndani ya nyumba”,amefafanua.

Akifafanua zaidi,  Sirima amesema utamaduni uliorithiwa kutoka kwa mababu wa kuwatumikisha wanawake kama watumwa unachangia kudhoofisha afya za wanawake kwa hiyo unapaswa kuachwa kwa lengo la kudumisha usawa wa jinsia.

No comments:

Post a Comment