Thursday, August 22, 2013

Wazawa wa mkoa wa Singida wenye uwezo washauriwa kuwekeza mkoani humo ili kuuletea maendeleo.

                                                   Bango la Katala Beach Hotel.
Sehemu ya majengo ya Katala Beach Hotel iliyopo kandokando ya Ziwa Singidani.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru mwaka huu Juma Ali Simai (wa sita kutoka kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkurungezi Mkuu wa Katala Beach Hotel bw. Kitila Katala (mstari wa mbele mwenye koti rangi ya kijivu) pamoja na viongozi mbalimbali na wananchi wa manispaa ya Singida. 

Mkurugenzi Mkuu wa Hoteli ya Katala Beach ya mjini Singida Kitila Katala, amewataka wazawa wa mkoa wa Singida walioko nje ya mkoa wenye uwezo kiuchumi, kuangalia uwezekano wa kuwekeza vitenga uchumi mbalimbali ili kuharakisha upatikanaji wa maendeleo katika mkoa wao.

Katala ametoa changamoto hiyo wakati akizungumza juu ya umuhimu wa wazawa wa mkoa wa Singida walioko nje ya mkoa, kushirikiana na ndugu zao kuuendeleza mkoa wa Singida ili usiendelee kubaki nyuma kimaendeleo.

Amesema uzoefu unaonyesha wazi kwamba wazawa wengi wa mkoa wa Singida wenye uwezo kiuchumi, wamekuwa wakiwekeza nje ya mkoa wao, kitendo kinachochangia mambo mengi ikiwemo mkoa kuendelea kuwa wa kwanza nchini kwa sifa ya umaskini.

Amesema ili mkoa uweze kupiga hatua kimaendeleo ikiwemo kuondoa sifa mbaya ya kuwa mkoa wa kwanza kwa umaskini ni lazima wazawa wa mkoa wa ndani na nje ya mkoa, kushikamana na kushirikiana katika kuuletea mkoa maendeleo endelevu yanayokwenda na wakati.

Kuhusu hotel yake ya Katala Beach, Mkurugenzi huyo amesema anatarajia ujenzi wa hotel yake hadi utakapokamilika, utamgharimu zaidi ya shilingi bilioni 2.5.

Hotel hiyo ya Katala Beach iliyopo kando kando ya ziwa Singidani, imezinduliwa rasmi na kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru Juma Ali Simai Agosti 21 mwaka huu.


Simai alimpongeza Katala kwa uamuzi wake wa kuwekeza mkoani kwake na kudai kuwa kitendo hicho ni cha kizalendo mno, na kuwataka wazawa wengine wa mkoa wa Singida kuiga uzalendo ulioonyeshwa na Katala wa kuendelea mkoa wake.

No comments:

Post a Comment