Friday, April 11, 2014

TANROADS Singida yatumia zaidi ya sh 5.1 B kutengeneza barabara zake Julai mwaka jana na februari mwaka huu.

Mkuu wa mkoa wa Singida na mwenyekiti wa bodi ya barabara, Dk.Parseko Vicent Kone, akifungua kikao cha bodi ya barabara cha 36 kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa VETA mjini Singida. Kulia (aliyekaa) ni katibu tawala mkoa wa Singida,Liana Hassan.
Meneja wa wakala wa barabara mkoa wa Singida (TANROADS), Mhandisi Yustaki Kangole, akitoa ufafanuzi juu ya sheria zinazotawala akiba/hifadhi  ya barabara kwenye kikao cha 36 cha bodi ya barabara mkoa wa Singida.
Mbunge wa jimbo la Manyoni Magharibi, John Lwanji akichangia hoja kwenye kikao cha 36 cha bodi ya barabara mkoa wa Singida kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano cha VETA mjini Singida.
Mkuu wa wilaya ya Mkalama, Edward Ole Lenga, akichangia hoja kwenye kikao cha 36 cha bodi ya barabara mkoa wa Singida kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa VETA mjini Singida.

Baadhi ya wajumbe wa bodi ya barabara mkoa wa Singida, waliohudhuria kikao cha 36 cha  bodi ya barabara mkoani Singida kilichofanyika  kwenye ukumbi wa mikutano cha VETA mjini Singida.

WAKALA wa barabara (TANROADS) mkoa wa Singida, umetumia zaidi ya shilingi 5.1 bilioni kugharamia matengenezo mbalimbali ya barabara zake kwa kipindi cha kati ya Julai mwaka jana na Februari mwaka huu.

Hayo yamesemwa na meneja wa TANROADS mkoa wa Singida, Mhandisi Yustaki Kangole, wakati akitoa taarifa yake ya utekelezaji na makadirio ya mpango kwa mwaka 2014/2015 mbele ya kikoa cha 36 cha bodi ya barabara.

Amesema matengenezo ya kawaida kwa barabara za lami, yametumia zaidi ya shilingi 409.8 milioni,wakati matengenezo ya kawaida kwa barabara za changarawe, zimetumia zaidi ya shilingi bilioni moja.

“Kwa upande wa sehemu korofi (lami), tumemia zaidi ya shilingi 52.5 milioni, barabara za changarawe shilingi 536.5 milioni”, amefafanua mhandisi Kangole.

Aidha, amesema katika kipindi hicho matengenezo ya vipindi maalum (lami), wametumia zaidi ya shilingi
356.5 milioni na kwa upande wa barabara za changarawe zaidi ya shilingi 1.1 bilioni zimetumika na matengenezo ya madaraja mbalimbali yametumia zaidi ya shilingi 1.6 bilioni.

Mhandisi Kangole amesema matengenezo hayo ni sawa na asilimia 46.7 ya bajeti yote ya mwaka wa fedha wa 2013/2014.

Kuhusu bajeti ya mwaka wa fedha wa mwaka ujao wa 2014/2015,mhandisi Kangole amesema wamekadiria kutumia zaidi ya shilingi 14.5 bilioni.

Kati ya fedha hizo, shilingi 4.4 bilioni zinakadiriwa kugharamia matengenezo ya kilomita 600 za barabara kuu na na madaraja 42.Zaidi ya shilingi 10.1 bilioni 10.1 bilioni zimekadiriwa kugharamia matengenezo ya kilomita 1,156 za barabara za mkoa na madaraja 58.


Wakala wa barabara (TANROADS ) mkoa wa Singida,inahudumia jumla ya kilomita 1,689.5 za barabara kuu na barabara za mkoa.Kati ya hizo,kilomita 371.9 ni za lami sawa na aslimia 22 na sehemu iliyobaki yenye kilomita 1,317.6 sawa na aslimia 78,ni barabara za changarawe au udongo.

No comments:

Post a Comment