Sunday, May 4, 2014

Mkapa awataka watanzania kuandika katiba itakayodumisha amani.

Rais mstaafu wa awamu ya tatu,Benjamen Williamu Mkapa (mwenye fimbo), akipokewa na mkuu wa mkoa wa Singida,Dk.Parseko Kone (wa pili kulia) kwenye viwanja vya zahanati ya kijiji cha Senenemfuru tarafa ya Mtinko wilaya ya Singida.Wa kwanza kushoto ni mwenyekiti CCM wilaya ya Singida, Narumba Hanje na anayefuatia ni mkuu wa wilaya ya Singida, Queen Mlozi.

Rais mstaafu Mkapa ambaye pia ni msarifu wa taasisi ya Benjamin William Mkapa HIV/AIDS foundation (BMAF),jana amekabidhi nyumba 30 za watumishi wa afya mkoani Singida zilizogharimu zaidi ya shilingi 1.9 bilioni.
Rais mstaafu Benjamin William Mkapa, akivishwa mgorole na wazee wa kata ya Ughandi wilaya ya Singida, muda mfupi kabla ya kuzungumza na wananchi waliohudhuria hafla ya kukabidhi nyumba 30 za watumishi wa zahanati mkoa wa Singida.
Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin William Mkapa, akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi nyumba 30 za watumishi wa zahanati,zilizojengwa na taasisi yake.Hafla hiyo imefanyika kwenye viwanja vya zahanati ya kijiji cha Senenemfuru wilaya ya Singida.
Afisa mtendaji mkuu wa taasisi ya Benjamin William Mkapa HIV/AIDS foundation (BMAF), Dk.Ellen Mkondya Senkoro,akitoa taarifa yake kwenye hafla ya kukabidhi nyumba 30 za watumishi wa zahanati zilizojengwa na taasisi hiyo ya Mkapa.
Mkuu wa mkoa wa Singida, Dk.Parseko Kone, akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi nyumba 30 za watumishi wa zahanati zilizojengwa na taasisi ya Benjamin Mkapa.Hafla hiyo imefanyika kwenye viwanja vya zahanati ya Senenemfuru wilaya ya Singida.
Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin William Mkapa, akipeana mkono na mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya ujenzi ya C.F.Bulilders LTD ya jijini Mwanza, Ferdnard Chacha, muda mfupi baada ya kukagua nyumba ya kuishi mtumishi wa zahanati ya kijiji cha Senenemfuru, iliyojengwa na taasisi ya Benjamin William Mkapa.

RAIS Mstaafu wa awamu ya tatu,Benjamin William Mkapa amewaasa Watanzania kuwa makini na waagalifu wakati huu wa mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya ili lengo la kupata katiba itakayoendelea kudumisha amani,upendo,utulivu na ushirikiano liweze kufikiwa.

Mkapa ametoa wito huo hivi karibuni wakati akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi nyumba bora 30 za watumishi wa vituo vya huduma ya afya mkoani hapa, nyumba hizo zimejengwa kwa zaidi ya shilingi 1.9 bilioni na taasisi ya Benjamin William Mkapa HIV/AIDS foundation (BMAF).

Amesema kuwa kunaweza kuwepo kwa kuhitalifiana lakini kamwe kusiwepo na kupigana au kufarakana kwa namna yoyote ile.


“Vyovyote mchakato wa katiba utakavyoishia tuhakikishe tunabaki na amani na utulivu wetu kwa ajili ya ustawi wa nchi yetu tuhitalifiane bila kupigana”,alisisitiza.

Alisisitizia zaidi hoja yake hiyo,Mkapa amesema Watanzania wanapaswa kwa pamoja kuhakikisha hawajiharibii nchi yao na zaidi wahakikishe kizazi cha sasa na kile kijacho kinaendelea kuwaenzi waasisi wetu kwa uadilifu mkubwa.

Kuhusu kukabidhi nyumba hizo 30 bora za watumishi wa afya,amesema anafarijika kufahamu kwamba wananchi wanaohudumiwa na zahanati 15 ambapo
nyumba 30 zimejengwa na taasisi yake wataendelea kufaidika na huduma bora za afya kwa sababu watoa huduma wameboreshewa mazingira ya kazi.

“Kama mnavyoona nyumba hizi ni za kisasa zina maeneo muhimu yote yanayokidhi mahitaji ya binadamu zipo imara na zimekidhi viwango vya ujenzi vinavyostahili, Kwa umahiri huu wa nyumba zilizojengwa napenda kumpongeza mkandarasi wake ambaye ni Mtanzania mzalendo C.F.Builders ltd na msimamizi mshauri wa ujenzi Y/P Architrcts (T) ltd”,amesema.


Aidha,ameziagiza halmashauri kuhakikisha nyumba hizo zinatumika kama inavyotarajiwa na kutunzwa vizuri ili ziweze kudfumu kwa muda mrefu.

Mkapa amezitaka pia zitenge bajeti ya kutosha kwa ajili ya kugharamia matengenezo madogo madogo pale yanapohitajika,ili ziweze kubaki katika hali ya kuvutia.

Vijiji vilivyonufaika na maradi huo katika wilaya ya Singida vijijini,ni Misughaa,Mnag’onyi,Mkenge,Mpambaa na Senenemfuru.Kwa upande wa wilaya ya Iramba,ni Ndago,Ulemo,Uwanza,Kinyambuli na Dominiki.


Willaya ya Manyoni ni Itigi,Idyondyandole,Elettra Bosco (Heka),Mpola na Chibumangwa.

No comments:

Post a Comment