Sunday, May 11, 2014

Singpress yatoa msaada wa zaidi ya laki nane kwa Walemavu Siku ya Uhuru wa Habari.

Mwalimu mkuu shule ya msingi mchanganyiko Ikungi waliya ya Ikungi, Olivary Kamilly, akizungumza ofisini kwake na wanachama wa klabu ya waandishi mkoa wa Singida, ambapo kwa kuadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, walitoa msaada wenye thamani ya zaidi ya shilingi laki nane kwa wanafunzi walemavu wakiwemo Albino katika shule hiyo.
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi mchanganyiko Ikungi wilaya ya Ikungi, Olivary Kamilly (wa pili kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wananchama wa Singida Press Club (Singpress).Wa tatu kulia ni mwenyekiti wa Singpress, Seif Takaza na wa kwanza kushoto ni mweka hazina wa Singpress na anayefuatia ni makamu mwenyekiti Damiano Mkumbo.
Mwanafunzi wa darasa la sita katika shule ya msingi mchanganyiko Ikungi wilaya ya Ikungi, Julius Charles, akionyesha umahiri wake katika kutumia vidole vya mguu wa kulia kuandika viruzi herufi kubwa na ndogo.Mwanafunzi huyo ambaye hana mikono, anafanya vizuri katika masomo yake.
Makamu mwalimu mkuu wa pili kitengo cha walemavu katika shule ya msingi mchanganyiko Ikungi,Donard Adamu Bilali, akizungumza na wanachama wa Singida Press Club, waliotembelea shule hiyo na kutoa msaada wa zaidi ya shilingi laki nane, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari.

WANACHAMA wa klabu ya waandishi wa habari (Singpress) mkoa wa Singida wameadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani kwa kutoa msaada wenye thamani ya zaidi ya shilingi laki nane kwa wanafunzi wenye ulemavu mbalimbali wakiwemo wenye ulemavu wa ngozi (albino).

Wanafunzi walionufaika na msaada huo ambao ni pamoja na sembe kilo 100,sukari kilo 50 na mchele kilo 150 ni wa shule ya msingi mchanganyiko Ikungi wilaya ya Ikungi mkoani Singida.

Akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi msaada huo,Mwenyekiti wa Singpress,Seif Takaza amesema katika kuadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani mwaka huu,klabu ya Singpress kwa dhati kabisa imeamua kushirikiana na wanafunzi walemavu wa shule ya msingi mchanganyiko Ikungi.


Akifafanua,Takaza amesema lengo na madhumuni ni kuwapatia wanafunzi walemavu zawadi na msaada mbalimbali ya kibinadamu ili waendelee kuamini kuwa na wao ni sehemu ya Watanzania.Vile vile kuwapunguzia makali ya maisha.

“Pia tunatarajia wanafunzi na walimu wa shule hii ya Ikungi,leo wanaweza kutumia fursa ya uwepo wetu kupaza sauti zao kwa kutoa chanagamoto na kero zinazowakabili,ili sisi tuweze kutekeleza jukumu letu la kuyaanika hadharani na jamii na serikali kwa ujumla iweze kuyatafutia ufumbuzi wa kudumu”amesema Takaza ambaye ni mwandishi wa habari wa gazeti la Mtanzania kwa mkoa wa Singida.

Akiongezea nguvu hoja yake hiyo,amesema waandishi wa habari wakiwemo wa Singpress jukumu lao ni
kufichua,kuonya,kuelimisha,kuburudisha na kukemea aina yoyote ya ukatili,unyanyasaji na unyanyapaa wanaofanyiwa watu wenye ulemavu.

Awali mwalimu wa shule hiyo,Olivary Kamilly alitaja baadhi ya changamoto wanazozikabili kuhusiana na wanafunzi walemavu,ni kukosekana kwa mafuta maalum ya ngozi (skin lotion),kupatikana maji kwa uhakika hapa shuleni na ukosefu wa kompyuta maalum kwa wanafunziwenye ulemavu wa macho,ili kwenda na mfumo wa mawasiliano uliopo hivi sasa duniani.


Aidha,amesema matarajio yao ni kuongeza ufanisi zaidi katika kuwasaidia wanafunziwenye ulemavu waweze kujitegemea na kuonyesha vipaji vyao katika kujenga maisha yao.

“Pia tunawapatia mafunzo ya ujasiriamali wanafunzi wenye ulemavu,ili kupunguza utegemezi pindi wamalizapo masomo yao”,amesema mwalimu Kamilly.

Mkuu huyo wa shule,ametumia fursa hiyo kuipongeza klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Singida,kwa uamuzi wao wa kiungwana kwa kuwasaidia wanafunzi walemavu ambao wapo kwenye kundi la watu wenye mahitaji maalum.

“Naomba nitumie fursa hii adimu,kuziomba asasi mbalimbali na watu binafsi kuiga mfano wa Singpress.Tuondoe dhana potofu kuwa misaada inatolewa na matajiri,makampuni makubwa au kutoka nje ya nchi,bali tushikamane sisi wenyewe bila kujali uwezo,tusaidie makundi haya hata kama msaada ni mdogo kiasi gani”amesema.


Kwa mujibu wa mwalimu Kamiily shule hiyo imeanzishwa mwaka 1944 kwa lengo la kutoa elimu ya msingi ya kawaida.Mwaka 1980,ilibadilishwa na kuwa shule ya msingi mchanganyiko ambapo kwa sasa ina wanafunzi 1,200 kati yao walemavu ni 104.

No comments:

Post a Comment