Thursday, May 1, 2014

Wakulima wapongezwa kwa kupanua kilimo cha mazao ya chakula.

MKUU wa Mkoa wa Singida,Dk.Parseko Vicent Kone amewapongeza wakulima kwa kuongeza juhudi ya kupanua kilimo cha mazao ya chakula na biashara msimu huu ikilinganishwa na misimu iliyopita.

Dk.Kone ametoa pongezi hizo wakati akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa chanjo kimkoa,iliyofanyika katika kijiji cha Mtinko jimbo la Singida kaskazini.

Amesema juhudi hizo za wakulima pamoja na kiwango cha mvua iliyonyesha cha mm 562 msimu huu kunaashiria kutakuwa na mavuno mengi mwaka huu.

Akiijengea nguvu hoja yake hiyo,Dk.Kone amesema hadi machi mwaka huu,jumla ya hekta 457,468 za mazao ya chakula na hekta 263,709 za mazao ya biashara zimelimwa.

“Mtarajio ni kuvuna tani
788.331 ya mazao ya chakula na tani 352,813.5 ya mazao ya biashara”,amesema.

Aidha,alitaja baadhi ya mazao ya chakula na matarajio ya tani zitakazovunwa kwenye mabano kuwa ni mtama (277,856.7),uwele (149,010.5),mpunga (11,108.22) na viazi vitamu (126,883).

Kwa upande wa mazao ya biashara,alitaja alizeti (216,360.5),ufuta (12,205.65),karanga (29,506.15),vitunguu (62,790.8),pamba (6,807.9),ulezi (13828) na tumbaku (2,892).

Katika hatua nyingine, amesema hali ya chakula imezidi kuimarika kwa kuwa baadhi ya mazao ya mwaka huu yameanza kutumika.

Amesema wananchi wameendelea kuhimizwa kutumia chakula watakachokipata kwa uangalifu mkubwa na kwa kutumia kadi ya usalma wa chakula ngazi ya kaya na kuzingaria matumizi muhimu ya chakula.

No comments:

Post a Comment