Tuesday, April 9, 2013

Polisi mkoani Singida yafanikiwa kumkamata mkulima akilimiki Bunduki ya Kijeshi aina ya SMG.

 Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Singida, ACP Linus Sinzumwa akitoa taarifa ya tukio la kukamata bunduki ya kijeshi SMG kwa waandishi wa habari (hawapo kwenye picha). Bunduki hiyo inayodhaniwa kutumika kwenye matukio ya uhalifu, imekamatwa katika kijiji cha Mwamangembe jimbo la Manyoni magharibi.
Afisa upelelezi wa makosa ya jinai (RCO) mkoa wa Singida, Thobias Sedoyeka (wa kwanza kulia) akifuatilia taarifa ya kukamatwa kwa bunduki ya kijeshi aina ya SMG  iliyokuwa ikitolewa na kamanda wa polisi mkoa wa Singida,Linus Sinzumwa.

Jeshi la polisi mkoani Singida, limefanikiwa kukamata bunduki ya kijeshi aina ya SMG na risasi zake 28, inayodhaniwa kuwa hutumika katika matukio ya uhalifu.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Singida Linus Sinzumwa amesema bunduki hiyo wameikamata Aprili saba  saa saba usiku katika kijiji cha Mwamangembe tarafa ya Itigi jimbo la Manyoni magharibi.
Sinzumwa ambaye amehamishiwa mkoani Mtwara amesema kuwa wameikamata bunduki hiyo ambayo ilikuwa ikimilkiwa na mkulima John Bobo (46) mkazi wa kijiji cha Mitundu, jimbo la Manyoni magharibi.
Akifafanua amesema baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia mwema juu ya mtuhumiwa huyo kumiliki bunduki hiyo ya kijeshi, waliweka
mtego uliofanikisha kukamatwa mtuhumiwa.
Sinzumwa amesema “Tumemkamata  mtuhumiwa alipokuwa anatoka katika nyumba aliyofikia katika kijiji cha Mwamagembe akielekea kufanya uhalifu saa hizo za usiku mnene kwa kutumia bunduki hiyo”.
Wakati huo bunduki hiyo yenye namba ya usajili 56-13207716, alikuwa ameihifadhi ndani ya mfuko wa salifeti.
Amesema kwa sasa wanaendelea kufanya upelelezi zaidi juu ya mkulima huyo kumiliki bunduki ya kijeshi na mara watakapomaliza, watamfikisha mtuhumiwa mahakamani ili kujibu tuhuma inayomkabili.
“Kule wilaya ya Manyoni,tunaendelea kupepeleza juu ya silaha nyingi kuzagaa katika wilaya hiyo.
Lengo letu ni kwamba tupate taarifa sahihi zitakazotusaidia kumaliza tatizo la kuzagaa kwa sihala hizo, zinazotumiwa katika ujangili na ujambazi”alisema.
Kamanda Sinzumwa alitumia fursa hiyo kuwashukuru na kuwapongeza wananchi kwa ushirikiano wao na jeshi la polisi na amewaomba wasichoke kutoa ushirikiano huo, ili mkoa wa Singida uendelee kuwa mji wa amani na utulivu.

No comments:

Post a Comment