Tuesday, April 9, 2013

Wilaya mpya ya Mkalama mkoani Singida yafanikiwa kuwapeleka shuleni wanafunzi 1,500 kati ya 1532.

Mkuu wa wilaya mpya ya Mkalama mkoani Singida, Edward Ole Lenga akihimiza shughuli za maendeleo katika mkutano wa hadhara uliofanyika  katika kijiji cha Gumanga kata ya Nduguti.

Wilaya mpya ya Mkalama mkoani Singida imefanikiwa kuwapelekea shuleni wanafunzi 1,500 ambao walikuwa hawajaripoti kuanza kidato cha kwanza mwaka huu katika shule walizopangiwa.
Hayo  yamesemwa na mkuu wa wilaya hiyo Edward Ole Lenga, wakati akizungumzia juu ya zoezi la kuwasaka wanafunzi 1,532 ambao hawakuripoti kuanza kidato cha kwanza Januari mwaka huu kama walivyopangiwa.
Amesema juhudi za makusudi zilizofanywa na viongozi na watendaji mbalimbali wa wilaya hiyo, zimefanikisha zoezi hilo la muda mfupi kwa asilimia kubwa.
Lenga amesema kazi bado inaendelea ya kuwasaka wanafunzi 32 ambao
hadi sasa bado hawajaripoti katika shule walizopangiwa.
Watu watakaobainika kusababisha wanafunzi hao kushindwa kuanza kidato cha kwanza mwaka huu sheria kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Akifafanua zaidi juu ya tatizo hilo, mkuu huyo wa wilaya amesema kuwa kata ya Ibaga hali ni mbaya zaidi kwa madai kuwa wanafunzi 20 hadi sasa bado hawajaripoti kuanza kidato cha kwanza.
Wakati huo huo, mkuu huyo wa wilaya amesema ujenzi wa vyumba vitatu vya maabara kwa kila shule 17 za sekondari wilayani humo, unaendelea vizuri na unatarajiwa kukamilika kabla ya septemba mwaka huu.

No comments:

Post a Comment