Thursday, November 14, 2013

Wajasiriamali wahimizwa kujitangaza kupitia vyombo vya habari.

Mkuu wa wilaya ya Singida,Queen Mlozi akizungumza kwenye hafla ya ufungaji wa mafunzo ya ufugaji bora nyuki iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa SIDO mjini Singida.Kulia ni meneja wa SIDO mkoa wa Singida, Shoma Kibende.
Meneja wa SIDO mkoa wa Singida,Shoma Kibende akitoa taarifa yake kwenye hafla ya ufungaji mafunzo ya ufugaji nyuki iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa SIDO mjini Singida.Wa pili kulia (aliyeketi) ni mkuu wa wilaya ya Singida,Queen Mlozi.
Mkuu wa wilaya ya Singida,Queen Mlozi akimkabidhi mfugaji wa nyuki cheti cha kumaliza mafunzo ya ufugaji bora nyuki yaliyomalizika mwishoni mwa wiki mjini Singida.
Mkuu wa wilaya ya Singida,Queen Mlozi,(aliyeketi katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wafugaji Nyuki waliohitimu mafunzo ya ufugaji bora wa Nyuki.Wa kwanza kushoto (walioketi) ni meneja wa SIDO mkoa wa Singida,Shoma Kibende na kulia ni mwenyekiti wa wafugaji Nyuki.

Serikali wilayani Singida, imewahimiza wajasiriamali na wafanyabiashara kujenga utamaduni wa kutangaza bidhaa zao kwenye vyombo vya habari ili pamoja na mambo mengine, waweze kujipatia soko la uhakika.

Wito huo umetolewa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Wilaya hiyo Queen Mlozi,wakati akizungumza kwenye hafla ya ufungaji mafunzo ya ufugaji bora wa nyuki na uchakataji wa asali.

Akifafanua amesema ushindani mkubwa wa biashara uliopo hivi sasa,mfanyabiashara atakayefanikiwa ni yule tu ambaye atatangaza biashara yake kikamilifu.

Mlozi amesema biashara bila matangazo,ni sawa na mtu asiye na biashara kwa sababu bidhaa zake,hazitajulikana.

Amesema pamoja na kujitangaza huko,kwanza wahakikishe bidhaa zao zina kuwa na ubora unaohitajika na pia wahakikishe wanashiriki maonyesho yanayoandaliwa na SIDO kanda ya kati.

Awali meneja wa SIDO mkoa wa Singida,Shoma Kibende, amesema kuwa SIDO inao mpango wa
kuwaelimisha wafugaji na kuhakikisha uzalishaji wa zao la asali unazingatia ubora tangu mahali zao linapoanzia.

Kibende amesema ubora huo unaanzia eneo la ufugaji,uvunaji na ufungashaji,upatikanaji wa masoko ya ndani na ya nje ya nchi.


“SIDO imeona umuhimu wa kutoa mafunzo haya kwa kuzingatia kwamba walengwa tayari wameanza shughuli za ufugaji nyuki,ununuzi na uuzaji wa zao la asali”,alifafanua zaidi meneja Kibende.

No comments:

Post a Comment