Picha zote kutoka maktaba ya Singida Yetu Blog
SINGIDA ni moja kati ya mikoa ambayo ilikuwa inafanya vizuri katika mchezo wa riadha miaka ya 1980 na kutoa wanariadha mahiri ambao waliiwakilisha Tanzania katika mashindano mbalimbali ya kimataifa.
Mkoa huo ni wenye mandhari nzuri yenye mawe mawe pamoja na mto upande wa kushoto na kulia hususan pale unapofika mkoani hapo.
Hakika mkoa huu ni wenye vitu vingi, lakini kikubwa zaidi ni wakimbiaji wa riadha hususan maeneo ya Singida Vijijini ambako kama wakimbiaji hao wataweza kupewa vifaa maalumu kwa ajili ya kukimbia na wadau wa riadha wakajitokeza na kuchangia zaidi katika riadha, Tanzania itakuwa na medali nyingi na kupata heshima katika nchi mbalimbali duniani.
Nasema hivyo kwa sababu hivi karibuni Mbunge wa Singida Vijijini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu aliandaa mashindano ya riadha hususan vijijini kwa ajili ya kuibua vipaji kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Shrika la African Wildlife Trust (AWT), Pratic Patel.
Mbio hizo zilizojulikana kwa jina la Singida Marathon za kilometa 21, zilianza rasmi Novemba 9, mwaka huu kwa kushirikisha wakimbiaji zaidi ya 400 kutoka Singida Mjini na Singida Vijijini na zilianzia Kijiji cha Mitula, Kata ya Kinyagigi na kuishia Viwanja vya Shule ya Msingu Ntunduu (W) Singida Vijijini.
Mbio hizo zilikuwa za kilometa 21 ambazo ni nusu marathoni na kilometa 5 na mwisho kabisa ni kilometa 2.5 ambazo ziliwashirikisha watoto wa kiume na wa kike. Wakimbiaji walikuwa wamejiandaa wenyewe na walijiandikisha, lakini baadhi yao pamoja na kukabiliwa na ukosefu wa viatu, lakini waliweza kumudu hali hiyo kutokana na mazingira waliyokua nayo na kuonesha vipaji vyao vilivyowashangaza wengi.
Inawezekana kukimbia bila viatu ni jambo lisiloruhusiwa, lakini kutokana na mazingira yenyewe ya vijijini hali hiyo haikuwa kikwazo kwa wakimbiaji hao kukimbia bila viatu ila walionesha kuwa wana moyo na nia ya dhati kuonesha vipaji vyao hakika ilikuwa faraja kubwa kwao kwani mwisho wa siku waliweza kuibuka washindi na wengine wakapata kifuta jasho.
Washindi hao ni Paulo Itambi ambaye aliibuka mshindi wa kwanza kwa upande wa wanaume ambaye alipewa zawadi ya Sh 300,000, Emmanuel Samson wa pili (Sh 200,000) na Samwel Ikungi wa tatu (Sh 100,000). Kwa upande wa wanawake, mshindi wa kwanza Fabiola William (Sh 300,000), Zakia Abdallah (Sh 200,000) na Winfrida Hassani (Sh 100,000).
Mbio za kilometa tano, washindi ni Gabriel Garado (Sh 200,000), Deo Lazaro (Sh 100,000) na Jonas John (Sh 50,000) huku wanawake ni Neema Kisuda (Sh 200,000), Pascalina Silvesta (Sh 100,000) na Christina Yuda (Sh 50,000) ambao washindi wa kilometa 2.5 wakiwa ni Julita Antony (Sh 100,000), Editha Gabriel (Sh 50,000) na Magreth Bernado (Sh 25,000).
Wanaume walikuwa ni Petro Pascal mshindi wa kwanza na kupewa Sh 100,000, Baraka Sebastian (Sh 50,000), Haji Swalehe (Sh 25,000) huku washindi wengine 400 kila mmoja akipewa Sh 10,000. Baada ya washindi hao kukabidhiwa zawadi zao, Patel ambaye alikuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Naibu Waziri Nyalandu, alikabidhi pia medali mbalimbali kwa washindi hao.
Aidha, alitoa changamoto kwa
wananchi hao kuacha tabia ya kuua tembo, bali wanastahili kulindwa na kuhifadhiwa ili kukuza uchumi na kufungua milango ya ajira.
Hata hivyo, baadhi ya washindi walimshukuru Nyalandu kwa kuamua kuanzisha mashindano hayo maeneo ya vijijini ili kuibua vipaji na kutoa rai kwa wadau wa riadha mkoani humo pamoja na sehemu mbalimbali kuanzisha klabu za michezo ya riadha ili kuendeleza vipaji na kuibuavipaji vipya.
Fabiola ambaye ni mkimbiaji mashuhuri wa riadha na aliyeiletea sifa Tanzania, alisema awali alikuwa akikimbia mkoani Kilimanjaro, lakini hivi sasa yupo Singida ambako alihamia Singida Vijijini kwenye Jimbo la Nyalandu, ndio kwao alipozaliwa na anaona fahari kubwa kuona wilaya hiyo ina wakimbiaji wengi na ni wazuri, lakini bado wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vifaa kwa ajili ya kufanyia mazoezi.
Fabiola na wadau wengine wamemwomba Naibu Waziri pamoja na wadau wengine kushirikiana kwa pamoja ili kuanzisha klabu za michezo ya riadha ili kuibua vipaji vya wakimbiaji waliopo maeneo ya vijijini.
Alisema mkoa huo una wanamichezo wengi, lakini hakuna klabu za michezo hali inayosababisha baadhi ya wanariadha kufanya mazoezi bila ya kuwa na vifaa maalumu, lakini walimpongeza Nyalandu kwa kuanzisha mashindano hayo maeneo ya vijijini ili kuibua wanamichezo wengi watakaoweza kuutangaza mkoa huo pamoja na Tanzania kwa ujumla pale yanapotokea mashindano ya riadha ya ndani na nje ya nchi.
No comments:
Post a Comment