Wednesday, November 13, 2013

Jeshi la Polisi lamshikilia mtuhumiwa kwa kosa la kubaka Kikongwe.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Singida, ACP. Geofrey Kamwela akitoa taarifa kwa waandishi wa habari (hawapo kwenye picha) juu ya kijana mmoja Saidi Hamisi (34) kumbaka Kikongwe mwenye umri wa miaka 80 (jina tunalo).Inadaiwa baada ya mtuhumiwa kumaliza kumbaka kikongwe huyo, alilala fo fofo kutokana na kulewa kupindukia hadi alipokuja kukamatwa akiwa amelala kwenye kitanda cha Kikongwe akiwa hajitambui.

JESHI la Polisi Mkoa wa Singida linamshikilia mkulima mkazi wa kijiji cha Wibia tarafa ya Mungaa wilaya ya Ikungi Saidi Hamisi (34) kwa tuhuma ya kumbaka bibi kizee mwenye umri wa miaka 80 na kumsababishia maumivu makali katika sehemu zake za siri.

Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake, kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Singida, ACP Geofrey Kamwela, alisema tukio hilo la aibu na kusikitisha limetokea Novemba Sita mwaka huu huko katika kijiji cha Matongo kata na wilaya ya Ikungi.

Akifafanua, alisema siku ya tukio mtuhumiwa ambaye alikuwa katika kijiji cha Matongo kuwajulia ndugu zake hali, alikunywa kiwango kikubwa cha Pombe ya kienyeji na kupelekea amfanyie kitendo hicho cha kinyama Kikongwe huyo.

“Mtuhumiwa alitumia mwanya wa nyumba za Tembe kutokuwa na mlango imara na hivyo alivuta taratibu mlango uliotengenezwa kwa fito na
kuingia mahali alipokuwa amelala kikongwe huyo. Baada ya kutimiza azma yake, kutokana na kulewa kupindukia, mtuhumiwa alilala fo fofo huku akikoroma”,alisema.

Kamwela alisema baada ya kikongwe huyo kubaini kuwa mbaya wake amelala fo fofo hajitambui, aliweza kutuma wajukuu zake kwenda kutoa taarifa katika serikali ya kijiji cha Matongo.Viongozi hao waliwasiliana na polisi wa kituo cha polisi Ikungi kwa simu ambapo walifika haraka, na kumkuta mtuhumiwa bado anaendelea kuchapa usingizi.

Alisema kwa sasa wanaendelea na upelelezi na utakapokamilika,mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma inayomkabili.

Katika hatua nyingine, Kamanda Kamwela ametumia fursa hiyo kutoa wito kwamba wakazi wa mkoa wa Singida wahakikishe wanakunywa pombe kwa kiwango cha kawaida na wajihadhari kunywa Pombe kupitiliza kwa madai watashindwa kufanya maamuzi sahihi.


“Lile tangazo linalotolewa mara kwa mara na vyombo vya habari kwamba ‘Pombe ni noma’, lina ukweli mkubwa. Pombe nyingi ina madhara mengi na makubwa ikiwemo kufikia maamuzi ambayo si sahihi”,alisema.

No comments:

Post a Comment