Friday, November 29, 2013

WANANCHI ZAIDI YA 1,000 SINGIDA WACHOMEWA NYUMBA ZAO MOTO.

Baadhi ya wananchi wakiwa wamehamishia makazi yao chini ya mti uliopo kwenye korongo kijiji cha Handa mpakani mwa Wilaya ya Chemba na Singida Vijijini mara baada ya nyumba zao kuchomwa moto na askari polisi na wale wa kikosi cha kupambana na ujangili kwa madai ya kuvamia hifadhi ya msitu wa mgori 
Huyu ni mmoja wa watoto walionashwa na kamera yetu akiwa amelala hoi kwa kukosa chakula na huduma zingine, baada ya nyumba zao kuchomwa moto wakati wa operesheni ya kuwahamisha katika kitongoji cha Kazamoyo kwa madai ya kuvamia hifadhi, hata hivyo wananchi hao wameisha katika eneo hilo kwa zaidi ya miaka nane toka mwaka 2005 , lakini sheria ya kuingiza eneo hilo kwenye msitu wa hifadhi ya mgori ilifanyika mwaka 2007.

KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) wametakiwa kufika katika kitongoji cha Kazamoyo kijiji cha Nguamuhanga tarafa ya Mgori Wilayani Singida vijijini na kujionea unyanyasaji dhidi ya wananchi wakati wa zoezi la kuwaondoa katika hifadhi ya msitu wa mgori.

Hayo yamesemwa juzi katika kitongoji hicho na baadhi ya wananchi walioamua kuhamia kwenye korongo na kuishi chini ya miti kama digidigi kunusuru maisha yao kutokana na vipigo kutoka kwa wa kikosi cha kupambana na ujangili Wilaya ya Singida na askari polisi.

Wamesema ni vyema kituo hicho wakafika mapema ili kuona jinsi ambavyo binadamu wanavyoishi maisha ya shida na taabu kwenye eneo hilo kufuatia amri ya mkuu wa Wilaya ya kuhamishwa kwa muda mfupi.

Wamesema eneo hilo wameishi zaidi ya miaka nane na kujenga makazi bora bila matatizo yoyote, lakini jambo la ajabu ni baada ya Wilaya ya Chemba na Singida kuwekeana mipaka na kuonekana kuwa wako Singida.

“Wakati tuko kijiji cha Handa Wilaya ya Chemba, tuliishi bila matatizo lakini baada ya kuhamia singida ndipo mambo yalianza kubadilika na kuambiwa kuwa tuko eneo la hifadhi, hii ni ajabu sana , Wilaya moja tuliishi vizuri hii nyingine haitutaki sasa tuende wapi.” Alihoji mmoja wa kina mama.

Licha ya kukosa huduma muhimu kama vile maji, mahema, vyoo baadhi ya kina mama na watoto walionekana wakiwa katika huzuni kubwa huku wengine wakiangua vilio baada ya kuwaona waandishi wa habari wakidhani kuwa ni
askari.

Hata hivyo eneo hilo lina mbu wengi, jua kali na mbaya zaidi hivi sasa ni msimu wa mvua katika maeneo hayo, je swali la kujiuliza wataishije hapo wananchi hao zaidi ya 1,000 ambao nyumba zao zimechomwa moto.

Hata hivyo Mkuu wa Wilaya ya Singida Queen Mlozi amesema zoezi hilo linaendelea sanjari na kuhakikisha wanaondoka kwenye korongo hilo walimojificha.

Hivi karibuni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Lazaro Nyalandu alitembelea eneo hilo la kusitisha zoezi la kuwahamisha mpaka pale kamati ya kudumu ya huduma za kijamii ya baraza la madiwani watakapokutana kutoa maamuzi sahihi juu ya wananchi hao.


Hata hivyo agizo hilo la Naibu Waziri limepingwa vikali sana na mkuu wa Wilaya ya Singida Mwalimu Queen Mlozi kwamba Nyalandu hana mamlaka kisheria ya kusitisha zoezi hilo, na kwamba anayeweza kumwamuru kusitisha zoezi ni Mkuu wa Mkoa pekee na si vinginevyo.

No comments:

Post a Comment