Saturday, November 30, 2013

MWENYEKITI WA KIJIJI MBARONO KWA KUCHOMA MOTO NYUMBA MBILI (2).

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Singida, ACP. Geofrey Kamwela akitoa taarifa kwa waandishi wa habari (hawapo kwenye picha) juu ya kuwashikilia wanakijiji 25 wakazi wa kijiji cha Makunda tarafa ya Kinampanda wilaya ya Iramba,kwa tuhuma ya kuchoma nyumba mbili kutokana na ugomvi wa kugombea ekari 284 za ardhi.

JESHI LA POLISI Mkoa wa Singida linawashikilia watu 25 wakazi wa kijiji cha Makunda Kata ya Kyengenge tarafa ya Kinampanda Mkoa wa Singida kwa kosa la kuchoma moto nyumba mbili kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kutokana na ugomvi wa kugombea ekari 284 za ardhi.

Kati ya watuhumiwa hao mmoja ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Makunda, Bw Godfrey Ayubu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, ACP Geofrey Kamwela amesema tukio hilo limetokea Novemba 26 saa mbili asubuhi huko katika Kijiji cha Makunda.

Amesema siku ya tukio, watu wapatao 50 wakazi wa Kijiji cha Makunda wakiwa wanaongozwa na Mwenyekiti wa Kijiji Bw, Godfrey huku wakiwa wamebeba silaha za jadi walichoma moto nyumba ya Esau Talanzia (47) na kuteketeza mali yote iliyokuwemo ndani.

“Vitu vilivyoteketea kwa moto huo ni magunia sita ya mahindi, gunia mbili za alizeti, godoro moja, fedha taslimu 450,000 pamoja na mali zingine vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya Tsh 18 milioni”,amesema Kamwela.

Amesema nyumba nyingine iliyochomwa moto na kuteketeza mali ya zaidi ya shilingi laki saba ni ya Matayo Kizaberga mali ya Matayo iliyoteketea ni gunia nne za mahindi, debe moja la dengu na fedha taslimu laki tano.

“Chanzo cha tukio hilo ni mgogoro wa mashamba ambapo wanakijiji cha Makunda wanapinga Esau na Matayo kumilikishwa ekari 284 wakati sio wazawa wa kijiji hicho”,amesema Kamanda Kamwela.

Kamwela amesema uchunguzi zaidi bado unaendelea na mara baada ya kukamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

Katika tukio jingine, Kamwela amesema mjasiriamali mkazi wa Mwenge mjini hapa, Richard  Williamu (33) Novemba 26 mwaka huu saa 1.45 jioni alipigwa risasi tumboni na paja la kulia na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi.

“Watu watatu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi walifika kwenye duka la Richard na kuomba wauze vocha na walipoambiwa kuwa dukani hapo hakuna vocha walichomoa bunduki inayodhaniwa ni SMG na
kumpiga risasi tumboni na kusababisha utumbo utoke nje Pia risasi hiyo ilimjeruhi paja la kulia”,amesema.

Amesema Richard amelazwa katika hospitali ya mkoa na hali yake inaendelea vizuri Jeshi la Polisi linaendelea kuwasaka watuhumiwa ili waweze kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

No comments:

Post a Comment