Sunday, November 3, 2013

Maelfu wamzika Mzee Gallawa.

Makamu mwenyekiti CCM taifa Tanzania bara, Phillipo Mangula (wa kwanza kulia) anayefuata ni waziri mkuu mstaafu Edward Lowassa,Mkuu wa mkoa wa Singida, Dk.Parseko Vicent Kone na pili kushoto ni Waziri wa Afya Dk.Hussein Mwinyi,wakiwa kwenye msiba wa mwenyekiti mstaafu CCM mkoa wa Singida, Abdallah Sumbu Gallawa.
Baadhi ya waombolezaji waliohudhuria mazishi ya mwenyekiti mstaafu CCM mkoa wa Singida, Mzee Abdallah Sumbu Gallawa katika kijiji cha Samumba kata ya Ikungi.
Makamu mwenyekiti wa CCM taifa Tanzania bara, Phillipo Mangula akizungumza kwenye mazishi ya mwenyekiti mstaafu CCM mkoa wa Singida, Mzee Abdallah Sumbu Gallawa.
Waziri wa Afya, Dk.Hussein Mwinyi akizungumza kwenye mazishi ya mwenyekiti mstaafu CCM mkoa wa Singida,Abdallah Sumbu Gallawa.Dk.Mwinyi alileta ubaini wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
Mwili wa mwenyekiti mstaafu wa CCM mkoa wa Singida, Abdallah Sumbu Gallawa ukiingizwa kaburini.
Waziri wa Afya, Dk.Hussein Mwinyi akiweka mchanga ndani ya kaburi la mwenyekiti mstaafu wa CCM mkoa wa Singida,Abdallah Sumbu Gallawa aliyefariki dunia Oktoba 29 mwaka huu akipatiwa matibabu katika hospitali ya misheni ya kijiji cha Puma wilaya ya Ikungi.

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Philip Mangula amewaongoza maelfu ya wakazi wa Mkoa wa Singida na baadhi ya viongozi wa ngazi mbalimbali wakiwemo wa ngazi ya kitaifa kwenye mazishi ya Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Mkoa wa Singida Mzee Abdallah Sumbu Gallawa (79).

Mazishi hayo yanayodaiwa kuvunja rekodi ya kuhudhuriwa na  maelfu  ya waombolezaji yalifanyika nyumbani kwa marehemu katika kijiji cha Sambaru kata ya Ikungi wilaya ya Mkoa wa Singida.

Akizungumza muda mfupi kabla ya mazishi,Mangula alitoa salamu za rambi rambi kutoka kutoka kwa mwenyekiti CCM taifa na Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania,Dk.Jakaya Mrisho Kikwete ambazo aliwatakia kila la kheri familia ya marehemu mzee Sumbu katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo.

Amesema Mwenyekiti huyo wa CCM taifa,alitamani angekuwepo kwenye mazishi hayo lakini ameshindwa kutokana na majukumu ya kikazi nje ya nchi.

Akizungumzia juu yamzee Gallawa,Mangula amesema alikuwa kiongozi bora na aliyekuwa karibu zaidi na watu na ndio maana mazishi yake yamehudhuriwa na maelfu ya wananchi.

Awali akisoma wasifu wa marehemu Gallawa,mbunge wa jimbo la Singida mashariki,Tundu Lissu amesema mzee Gallawa ni mzawa wa kwanza wa mkoa wa Singida kuchaguliwa kuwa mkuu wa wilaya na alianzia kazi hiyo wilaya ya Mbulu mkoa wa Manyara kuanzia mwaka 1962-1965.

Mwaka 1965 aligombea ubunge wa wilaya ya Singida na
hakufanikiwa kushinda.Mwaka 1980 aligombea ubunge jimbo la Singida mjini na alishinda.

Mwaka 1992 akigombea nafasi ya mwenyekiti wa CCM mkoa wa Singida na kushinda.

Marehemu mzee Gallawa amezaliwa Novemba 1934 katika kijiji cha Sambaru Alianza kusoma katika shule ya msingi Ikungi mwaka 1945-1949,mwaka 1950 alianza masomo shule ya sekondari Mpwampwa mkoani Dodoma.

Baadhi ya viongozi wengine waliohudhuria mazishi hayo ni Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa waziri wa afya,Dk.Hussein Mwinyi,waziri kutoka Tamisemi, Kasimu Majaliwa (alimwakilisha waziri mkuu),naibu Waziri kilimo,Chakula na Ushirika,Adamu Malima,Naibu Waziri Mawasiliano,Eng.Dk.Charles Tizeba na Naibu Waziri Maendeleo ya Jamii,Jinsia na Watoto,Ummy Mwalim.

Wageni wengine ni wakuu wa mikoa,Dk.Rehema Nchimbi (Dodoma),Elaston Mbwilo (Manyara) na Mwantumu Mahinza (Pwani).Pia walikuwepo wakuu wa wilaya zaidi ya kumi.

Katika hatua nyingine, Mangula aliwasilisha ubani kutoka CCM taifa,shilingi 1,400,000/=,wabunge 12 wa mkoa wa Singida,shilingi 1,200,000/=,wabunge wa mkoa wa Tanga, shilingi 500,000/= na ofisi ya waziri mkuu shilingi 500,000/=.


Aidha,Waziri Dk.Mwinyi aliwasilisha ubani kutoka kwa Rais Kikwete ambao hata hivyo,idadi haikuweza kufahamika.Kwa mujibu wa Dk.Mwinyi yeye alikabidhiwa bahasha na hakuelezwa ilikuwa na kiasi gani cha ubani.

No comments:

Post a Comment