Monday, November 18, 2013

Wachimbaji wadogo wa madini watakiwa kulipa kodi bila shuruti.

Kamishina msaidizi Madini kanda ya Kati, Manase Mbasha akizungumza kwenye ufunguzi wa mafunzo ya siku tano ya uchimbaji bora wa Madini yanayohudhuriwa na wachimbaji wadogo 35 kutoka mikoa 15 nchini.Mafunzo hayo yanafanyikia kwenye ukumbi wa mikutano wa kanisa katoliki mjini Singida. Kulia ni afisa mwandamizi wa ofisi ya madini mkoa wa Singida, Gabriely Senge na kushoto ni mkufunzi wa mafiunzo hayo,Dk.Eng.Crispin Kinabo kutoka chuo kikuu cha Dar-es-salaam.

Baadhi ya wachimbaji wadogo wakifuatilia kwa makini mada zilizokuwa zikitolewa za mafunzo ya uchimbaji bora wa Dhahabu.

Wachimbaji wadogo wa madini nchini,wametakiwa kujenga utamaduni wa kulipa kodi bila kushurutishwa,ili kuisaidia serikali kuwa na uwezo wa kutoa huduma bora zinazokidhi mahitaji ya wananchi.

 Wito huo umetolewa na Kamishina Msaidizi Madini Kanda ya Kati,Manase Mbasha,wakati akizungumza kwenye hafla ya ufunguzi wa mafunzo ya siku tano ya uchimbaji bora wa dhahabu yanatoendelea kwenye ukumbi wa mikutano wa kanisa katoliki mjini hapa.

 Amesema lengo la serikali ni kuhakikisha wachimbaji wadogo wa madini,wanakuwa walipaji wazuri wa kodi kwa mujibu wa sheria zilizowekwa za sekta ya madini.

 “Mchimbaji mdogo ukiwa mlipa kodi mzuri,kwanza utajijengea heshima mbele ya macho ya jamii,na kikubwa zaidi ni kwamba utakuwa umeisaidia serikali kuwa na uwezo mzuri wa kuhudumia wananchi wake”alifafanua Mbasha.

 Aidha,kamishina huyo msaidizi,ametumia fursa hiyo kuwahimiza wachimbaji wadogo kushiriki kikamilifu shindano la tuzo ya rais ya mazingira.

 Mbasha amesema endapo wachimbaji wadogo na wale wa ngazi mbalimbali watashiriki kikamilifu katika shindano la tuzo ya rais ya mazingira, kitendo hicho kitasaidia mno kuboresha mazingira.

 Kwa mujibu wa Mkufunzi wa Mafunzo hayo,Dk.Eng.Crispin Kinabo kutoka chuo kikuu cha Dar-es-salaam kitengo cha Jiolojia,baadhi ya mada za mafunzo hayo,ni
mbinu za kufundisha wachimbaji ambao hawakubahatika kufika kwenye mafunzo hayo, sheria zinazotawala sekta ya madini na uchorogaji na kuchejua.


 Mafunzo hayo yanahudhuriwa na wachimbaji wadogo 35 kutoka mikoa 15.Mafunzo hayo yameandaliwa na kufadhiliwa na wizara ya nishati na madini na yanasimamiwa na kampuni za ushauri za Tandiscovery na Bureau for Industrial Cooperation.

No comments:

Post a Comment