Thursday, November 7, 2013

TRA Singida yazindua rasmi siku ya mlipa kodi.

Afisa elimu na huduma kwa mlipa kodi TRA mkoa wa Singida, Zakaria Gwagilo akitoa taarifa kwa waandishi wa habari (hawapo kwenye picha) juu ya maadhimisho ya saba ya siku ya mlipa kodi ambayo yamezinduliwa rasmi juzi. Zakaria alitoa taarifa hiyo kwa niaba ya kaimu meneja TRA mkoa wa Singida Alistides Paulo.

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Singida imezindua rasmi maadhimisho ya saba ya siku ya mlipa kodi Tanzania kwa kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo ya kutoa misaada kwa makundi yenye mahitaji maalumu.

Hayo yamesemwa na Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Singida, Alistides Paulo wakati akitoa taarifa yake kwa waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya saba ya siku ya mlipa kodi Tanzania kwa Mkoa wa Singida.

Katika taarifa yake hiyo iliyosomwa kwa niaba yake na Afisa Elimu na huduma kwa mlipa kodi Zakaria Gwagilo alitaja baadhi ya shughuli zitakazofanyika katika maadhimisho hayo kuwa ni pamoja na kutoa misaada kwenye wodi ya wazazi katika hospitali ya wilaya ya Manyoni.

Paulo alitaja shughuli zingine kuwa watafanya semina kwa makundi mbalimbali ya walipa kodi na pia kuwatembelea walipa kodi kwenye vituo vya biashara na kuzungumza nao kuweza kufahamu matatizo yao.

“Katika kilele cha siku ya mlipa kodi Novemba nane mwaka huu baadhi ya walipa kodi watazawadiwa vyeti kutokana na
kukidhi vigezo vya ubora wa kutunza kumbukumbu sahihi za biashara kulipa kodi sahihi na kwa wakati na ulipaji kodi kwa hiari”,amesema Kaimu Meneja huyo.

Kwa mujibu wa Kaimu Meneja Paulo mkoa wa Singida unatarajia kuongeza makusanyo kutoka shilingi 4.19 kwa mwaka 2013/2014 zinatajiwa kukusanywa hadi shilingi 8.3 bilioni ifikapo mwaka 2017/2018.


Kwa mwaka huu ujumbe wa siku ya mlipa kodi ni “Tulipe kodi kwa matokeo makubwa sasa”.

No comments:

Post a Comment