Monday, September 9, 2013

Shirika lisilo la kiserikali lakabidhi Zahanati na Nyumba zenye thamani ya Tsh 115.9 mkoani Singida

 Mkurugenzi wa shirika la HAPA, David Mkanje akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano ya Zahanati na nyumba ya watumishi ya kijiji cha Kinampundu wilaya ya Mkalama. Kulia wa nne ni mkuu wa wilaya ya Mkalama na wa kwanza kushoto ni katibu tarafa Nduguti wilaya ya Mkalama, Nyalandu.
 Mkurugenzi wa shirika la HAPA,David Mkanje (kushoto) akimkabidhi mkuu wa wilaya ya Mkalama, funguo za zahanati ya kijiji cha Kinampundu. HAPA imejenga zahanati hiyo na nyumba ya watumishi kwa gharama ya zaidi ya shilingi 115.9.
 Mkuu wa wilaya ya Mkalama,Edward Ole Lenga akifungua rasmi Zahanati ya kijiji cha Kinampundu.
Mkuu wa wilaya ya Mkalama mkoa wa Singida,Edward Ole Lenga akizungumza kwenye hafla ya kukabidhiwa zahanati ya kijiji cha Kinampundu.Wa kwanza kushoto ni mkurugenzi wa shirika la HAPA lililojenga zahanati hiyo kwa zaidi ya shilingi 115.9. Siku za nyuma wakazi zaidi ya 7,000 wa kijiji hicho, walikuwa wakitembea umbali wa zaidi ya kilomita 12 kufuata huduma ya afya.
Baadhi ya wageni kutoka Uholanzi, Amerika, Uingereza na Ireland waliohudhuria hafla ya makabidhiano ya zahanati na nyumba ya watumishi wa katika kijiji cha Kinampundu wilaya ya Mkalama.
Mkuu wa wilaya ya Mkalama Edward Ole Lenga akiwa na mwakilishi wa shirika la SIMAVI la nchini Uholanzi, Ljeke muda mfupi baada ya kuzindua nyumba ya watumishi wa zahanati ya kijiji cha Kinampundu.Wa pili kulia ni mkurugenzi wa shirika la HAPA, David Mkanje.

Shirika lisilo la kiserikali la Health Action Promotion Association (HAPA) la Mkoa wa Singida limetumia zaidi ya shilingi 115.9 milioni kugharamia ujenzi wa jengo la Zahanati na nyumba ya watumishi katika kijiji cha Kinampundu wilaya ya Mkalama.

Fedha hizo, pia zimetumika kununulia kitanda cha kuzalishia,vifaa vya kuzalishia, mizani ya watu wazima, mizani ya watoto wachanga, stendi ya drip na kitoroli cha kugawia dawa.

Hayo yamesemwa mwishoni mwa juma na Mkurugenzi wa HAPA, David Mkanje wakati akizungumza kwenye makabidhiano ya majengo hayo kwa uongozi wa wilaya ya Mkalama.

Alisema ujenzi wa jengo la zahanati pamoja na vyoo vyake, HAPA imetumia shilingi
54 milioni wakati mchango wa wananchi ni shilingi 14 milioni.

“Jengo la nyumba ya watumishi HAPA imetumia zaidi ya shilingi 11.8 milioni halmashauri ya wilaya ya Mkalama,imechangia zaidi ya shilingi 19.7 millioni na wananchi wa kijiji cha Kinampundu wamechangia zaidi ya shilingi 9.4″ million, amesema David.

Mkurugenzi huyo alisema fedha zilizotumiwa na HAPA ni ufadhili kutoka shirika la SIMAVI la nchini Uholanzi na Volunteers Africa kutoka Uingereza.

Akifafanua Bw. David amesema HAPA imeamua kuwapunguzia wananchi wa kijiji cha Kinampundu zaidi ya kero 7,000 ya kufuata huduma ya afya zaidi ya kilomita 12.

“Wananchi wa Kinampundu pamoja na wa vijiji vingine 61 ambako mradi huu unatekelezwa,mbali na kufuata huduma ya afya umbali mrefu, pia kipindi cha masika au usiku na miundo mbinu ya barabara kutokupitika kumechangia pamoja na mambo mengine wanawake wajawazito kujifungulia nyumbani. Hali hiyo imechangia vifo vya akina mama wajawazito na watoto”,amesema.

Katika hatua nyingine,Mkurugenzi David amesema pamoja na kukabidhi mradi huo wa zahanati, shirika la Hapa  chini ya ufadhili wa shirika la SIMAVI bado wanaendelea na utekelezaji mradi wa UFBR maarufu kwa jina la ‘Pamoja Tunaweza’. Mradi huu ni wa Afya ya Uzazi na Jinsia.


Akifafanua zaidi Bw.David amesema mradi huo unatekelezwa katika tarafa za Nduguti na Kirumi kwa wilaya ya Mkalama na tarafa ya Ndago kwa wilaya ya Iramba.

No comments:

Post a Comment