Friday, September 6, 2013

Walimu waaswa kuzingatia viapo katika usimamiaji wa mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi.

Mkuu wa shule ya msingi Ikungi mchanganyiko, Olivary Kamili akiagalia wanafunzi wakijipanga tayari kuingia madarasani kuanza masomo.

Mkurugenzi Mtendaji wa kwanza wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida,Magayane Protace,amewataka walimu watakaosimamia mtihani wa taifa wa darasa la saba mwaka huu,kujiepusha na vitendo ambavyo ni kinyume na viapo vyao.

Magayane ametoa tahadhari hiyo mwishoni mwa wiki,wakati akifungua semina iliyohudhuriwa na walimu wa shule za msingi tarafa ya Sepuka,wanaotarajiwa kusimamia mtihani wa taifa wa kumaliza elimu ya msingi mwaka huu.

Alisema kazi ya kusimamia mtihani wa taifa wa darasa la saba,ni lazima kila mwalimu ale kiapo mbele ya
hakimu kwamba hatafanya vitendo vitakavyokizana na sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.

Akifafanua zaidi,Protace alisema kiapo hicho ni kwamba pamoja na mambo mengine, mwalimu atatunza siri,hatawafundisha wala kuwaelekeza wanafunzi namna ya kujibu maswali ya mtihani.

“Kwa hali hiyo,mwalimu atakayekiuka au kwenda kinyume na kiapo chake,atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria za nchi “alisema na kuongeza;

“Kazi ya usimamizi wa mtihani mtakayoifanya,najua ni nzito sana na kamwe hailingani na posho mtakayolipwa.Lakini kwa vile serikali imewaamini,ifanyeni kazi hii kwa moyo wa kujitolea zaidi”.alisema Protace.


Wilaya mpya ya Ikungi,ina shule za msingi 97 na kati yake zenye darasa la saba,ni 94.Wanafunzi 4,740 wa wilaya hiyo,wanatarajiwa kufanya mtihani wa darasa la saba mwaka huu utakaofanyika septemba 11 na 12 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment