Saturday, September 7, 2013

WFP watoa msaada wa pampu za maji zenye thamani Tsh 94 millioni mkoani Singida

Mkuu wa Ofisi ndogo ya Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Dodoma, Nima Sitta akihimiza utunzaji wa matenki ya kuvunia maji ya mvua yaliyojengwa katika shule za msingi wilaya ya Singida na Ikungi. Shirika la WFP limetoa shilingi 95,271,600 kugharamia ujenzi wa matenki hayo.

Shirika lisilo la kiserikali la Mpango wa chakula duniani (WFP) limetoa msaada wa pampu 210 za maji zenye thamani ya zaidi ya shilingi 94 milioni kwa shule za msingi na vikundi mbalimbali mkoani Singida.

Pampu hizo ni kwa ajili ya kilimo cha umwangiliaji bustani.

Hayo yamesemwa juzi na Mkuu wa Ofisi ndogo ya WFP Dodoma Nima Sitta,wakati akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano ya matenki 12 ya kuvunia maji ya mvua yaliyojengwa kwenye shule sita za wilaya ya Singida na wilaya ya Ikungi.Hafla hiyo ilifanyika katika viwanja vya shule ya msingi Igaruri wilaya ya Singida.

Alisema lengo kuu la msaada huo wa pampu za maji,ni kila shule za msingi na vikundi vya vijana,kuanzisha
kilimo cha umwangiliaji maji bustani.

Nima alisema kila shule ya msingi yenye chanzo cha maji,itapatiwa pampu si chini ya mbili,wakati vikundi vya vijana waliomaliza elimu ya msingi na wale waliomaliza kidato cha nne,watapatiwa si chini ya pampu tatu.

“Kwa upande wa vijana,kila kikundi kinatakiwa kumiliki ekari sisizopungua tatu na wawe wamejipanga vizuri,shule za msingi zimepewa sharti la kuwa na shariti la kumiliki ekari mbili.Hivi sasa tunaendelea kuzizungukia shule ili zile zenye sifa,ziweze kukabidhiwa pampu mapema iwezekanavyo”alifafanua Nima.

Katika hatua nyingine,Nima alitumia fursa hiyo kulipongeza shirika lisilo la kiserikali la SEMA la mjini Singida, kwa kazi nzuri ya ujenzi wa matenki ya kuvunia maji na inayofanana na thamani ya fedha zilizotumika .

“Kwa kweli SEMA kazi yao ni nzuri mno,wametekeleza kwa kiwango cha juu yale yote ambayo yapo kwenye mkataba na kufanya mazuri zaidi baadhi ya shughuli ambazo hazipo kwenye mkataba.Nisema tu kwamba kazi ya SEMA,inapaswa kuigwa na wajenzi wengine kwa maendeleo ya wananchi”,alisema.

No comments:

Post a Comment