Monday, September 30, 2013

TANROADS Singida yatumia shilling 6.4 bilioni kugharamia matengenezo ya barabara.

 Mkuu wa mkoa wa Singida na mwenyekiti wa bodi ya barabara mkoa wa Singida, Dk.Parseko Kone akifungua kikao cha 35 cha bodi ya barabara kilichofanyika kwenye ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa mjini Singida.Wa kwanza kulia ni mwenyekiti wa CCM mkoa wa Singida, Mgana Izumbe Msindai na kushoto ni mbunge wa jimbo la Singida Magharibi Mohammed Missanga.
 Kaimu meneja wa TANROADS mkoa wa Singida, Eng.Yohannes Mbegalo (wa kwanza kushoto) akifuatilia kwa makini taarifa mbalimbali zilizokuwa zikijadiliwa kwenye kikao cha 35 cha bodi ya barabara mkoa wa Singida.
Baadhi ya wakuu wa wilaya za mkoa wa Singida waliohudhuria kikao cha 35 cha bodi ya barabara mkoa wa Singida kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano ofisi ya mkuu wa mkoa Singida.

WAKALA wa barabara (TANROADS) Mkoa wa Singida umetumia zaidi ya shilingi 6.4 bilioni katika kugharamia matengenezo mbalimbali ya barabara kuu za mkoa na madaraja katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu.

Hayo yamesemwa na Kaimu Meneja wa TANROADS, Mkoa wa Singida Eng.Yohannes Mbegalo wakati akitoa taarifa yake ya utekelezaji mbele ya kikao cha 35 cha bodi ya barabara mkoa kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu  wa mkoa mjini hapa.

Amesema fedha hizo zimetumika kugharamia matengenezo ya kawaida kwa upande wa barabara za lami na changarawe.

“Pia zimetumika kugharamia matengenezo ya sehemu korofi,matengenezo ya vipindi maalum.Matengenezo yote hayo yamefanyika kwenye barabara za lami na zile za changarawe Shilingi 1.5 bilioni zimetumika katika matengenezo ya madaraja mbalimbali”,amesema Kaimu Meneja huyo.

 Kwa upande wa miradi mikubwa, Mbegalo amesema barabara ya Manyoni-Itigi-Chaya mkoani Tabora inayojengwa kwa kiwango cha lami na mkandarasi Sinohydro Corporation kutoka China yenye urefu wa kilomita 89.3,ujenzi wake hadi Juni mwaka huu,ulikuwa asilimia 43.9 kulingana na mkataba,wakati kazi ilitakiwa iwe imefikia asilimia 89.

 “Mradi mwingine mkubwa wa ujenzi wa daraja la
Sibiti wilaya ya Mkalama ililopo mpakani mwa mkoa wa Singida na mkoa wa Simiyu lenye urefu wa meta 82,ujenzi wake unafanywa na mkandarasi Hainan International ltd.Mkandarasi hadi juni mwaka huu,amesafisha barabara yote ameanza ujenzi wa nguzo za daraja na makalavati kwa upande wa Singida”,amesema Mbegalo.

 Aidha, Kaimu Meneja huyo alisema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba mkubwa wa maji unaochangia baadhi ya sehemu za kazi kuchelezwa kuanza na pia kutokamilika kwa wakati uliopangwa.


 Wakala wa barabara mkoa wa Singida,unahudumia jumla ya kilomita 1,689.5 za barabara kuu na zile za mkoa.Kati ya hizo,kilomita 367.9 ni za lami sawa na aslimia 21.8 na sehemu iliyobaki yenye urefu wa kilomita 1,321.6 sawa na asilimia 78.3 ni za barabara za changarawe au udongo.

No comments:

Post a Comment