MKUU wa wilaya ya Singida,Queen Mwashinga Mlozi,amewatahadharisha madiwani na watendaji kata,kwamba kabla ya mei 30 mwaka huu wawe wamekamilisha ujenzi wa vyumba vitatu vya maabara,vinginevyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Mlozi ametoa agizo hilo wakati akizungumza mbele ya kikao cha kawaida cha baraza la madiwani kilichofanyika mjini Singida.
Alisema madiwani na watendaji kata ambao watashindwa kumaliza ujenzi huo kabla ya muda uliopangwa,watawajibishwa ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani.
“Nitafanya hivyo kwa mujibu wa mamlaka niliyopewa chini ya kifungu cha 14 na 15 vya sheria za tawala za mikoa na serikali za mitaa ya mwaka 2002 ya kuvunja amri halali ya kutokujenga vyumba vitatu vya maabara”alifafanu mkuu huo wa wilaya.
Dc Mlozi alitaja shule za kata ambazo ujenzi wake
umefikia asilimia 80,kuwa ni Mdasenga,Maghojoa,Ntoge,Mughunga,Makuro,Mrama,Mwanamwema,Ngimu,Nyeri na Itaja.
Katika hatua nyingine,alisema kuwa kampuni ya bia Tanzania (TBL) kwa kushirikiana na taasisi za fedha,imeazimia kufanya zao la mtama (mweupe),kuwa zao la kutumainiwa la biashara katika mkoa wa Singida.
Akifafanua,Mlozi alisema TBL inahitaji kununua tani 7,000 na ili kufikia lengo la upatikanaji wa tani hizo,taasisi za fedha za CRDB benki na NMB,zitashirikiana na wakulima ili kuhakikisha wanalima kitaalam kwa kutumia zana bora na kilimo cha kisasa.
“Madiwani na watendaji wote tutumie fursa hii kwa kuhakikisha tunawahamasisha wakulima wetu wanufaike na kilimo hiki cha mtama mweupe.Tujipange vizuri kwa utekelezaji”,alisema Mlozi.
No comments:
Post a Comment