Thursday, February 20, 2014

Diwani wa CCM kizimbani kwa lugha ya matusi.

Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini Singida.

DIWANI wa kata ya Unyambwa (CCM) Halmashauri ya Manispaa ya Singida,Shaban Salum Satu amepandishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi mjini Singida akituhumiwa kuwatolea lugha ya matusi maafisa wa Polisi ikiwemo kudai ni ‘mizigo’.

Diwani huyo alifikishwa mahakamani kwa kosa la kutoa lugha ya matusi hivi karibuni anatarajiwa kupandishwa tena kwenye mahakama hiyo kwa tuhuma ya kushiriki kuchoma moto basi la Mtei lililogongwa pikipiki iliyokuwa inatumiwa na watu wanne wa familia moja kwenda shambani.Wanafamilia watatu,walipoteza maisha papo hapo.

Baadhi ya lugha ya matusi inayodaiwa kutolewa na diwani huyo,ni “nyinyi wasege tu,
wapumbavu,hamna akili,vibaraka wa Mtei,mnakamata watu ovyo vyo mna njaa mnataka kuchukua shilingi elfu kumi kumi kwa wapiga kura wangu”.

Mwendesha mashitaka Chemu Mussa,alidai mbele ya hakimu Aisha Mwetindwa kuwa mnamo januari 12 mwaka huu saa 1.30 asubuhi huko katika kijiji cha Ijanuka kata ya Unyambwa tarafa ya Mungumaji manispaa ya Singida,mshitakiwa Shaban aliwatolea lugha ya matusi maafisa wa polisi kitendo kilichoelekea kusababisha kutoweka/kuvunjika kwa amani.

Amesema tukio hilo lilitokea wakati maafisa hao wa polisi walikuwa kazini wakilinda amani na utulivu kwenye eneo ambalo wananchi wa kata ya Unyambwa walichoma basi la kampuni ya Mtei.

Mshitakiwa amekana shitaka na yupo nje kwa dhamana ya shilingi laki tano had februari 25 mwaka huu,kesi yake itakapotajwa tena.

Wakati huo huo,Jamhuri inatarajia kuita mashahidi sita kutoa ushahidi dhidi ya mshitakiwa diwani Satu.

Mashahidi hao ni D/ssge Mohammed,F531 D/C Boniface,A/INSP.Hassan,D.9749,D/CPL.Ally,G.6041 D/C Sikitu na E.4998.D/CPL.Mohammed.

No comments:

Post a Comment