Sunday, February 16, 2014

Viongozi wa umma wahimizwa kushirikiana na wasimamizi wa utafiti.

Baadhi ya wadadisi na wasimamizi wa utafiti wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi 2014 wakisikiliza mada zilizokuwa zikitolewa kwenye mafunzo yao yaliyomalizika mjini Singida.Wadadisi na wasimamizi hao wametoka mkoa wa Kigoma,Tabora,Singida na Dodoma.
Katibu tawala mkoa wa Singida,Lina Hassan (wa pili kulia walioketi) akiwa kwenye picha ya pamoja na wadadisi na wasimamizi wa utafiti wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi mwaka 2014.Kushoto ni Afisa takwimu mkoa wa Singida Mazinza na anayefuata ni mwakilishi wa mkurugenzi mkuu,ofisi ya taifa ya takwimu Bakilla Bakilla na kulia ni mwakilishi wizara ya kazi na ajira,Thomas Saguda.

VIONGOZI wote wa serikali na wa ngazi zote katika mikoa ya Kigoma,Singida,Tabora na Dodoma,wamehimizwa kutoa ushirikiano,kuhamasisha na kuelimisha umma, umuhimu wa kushirikiana na wadadisi na wasimamizi wa utafiti wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi wa mwaka 2014.

Imedaiwa kuwa hatua hiyo itasaidia kufikiwa kwa urahisi kwa lengo la serikali ambalo ni kujua soko la ajira nchini lilivyo hivi sasa.

Wito huo umetolewa juzi na Katibu Tawala mkoa wa Singida,Liana Hassan wakati akizungumza kwenye ufungaji wa mafunzo ya siku 14 ya wadadisi na wasimamizi wa utafiti wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi mwaka 2014.Wadadisi na wasimamizi hao,wametoka mikoa ya Kigoma,Tabora,Singida na Dodoma.

Amesema umma wakijua umuhimu wa utafiti huo,watakuwa tayari kutoa
ushirikiano wa hali ya juu utakaosaidia lengo la utafiti kufikiwa kwa urahisi.

“Kwa upande wenu na ninyi wadadisi na wasimamizi wa utafiti huu,nendeni mkaifanye kazi yenu kwa uadilifu na weledi mkubwa,kwa njia hiyo,umma utawapa ushirikiano mzuri na mtapewa takwimu mnazozihitaji kwa wepesi zaidi”alisema na kuongeza;

“Ni matumaini yangu kwamba,wadadisi mmepata mafunzo madhubuti na ya kina ambayo yatawawezesha kuweza kukusanya takwimu hizi zinazotakiwa sana na taifa letu,katika kuangalia hali ya soko la ajira nchini,kwa umahiri mkubwa”.

Awali Mwakilishi wa Mkurugenzi mkuu,ofisi ya taifa ya takwimu,Bakilla Bakilla amesema taarifa zitakazokusanywa kutoka katika kaya pamoja na taarifa binafsi za wanakaya,zitatunzwa kwa usiri mkubwa kama inavyotakiwa kwa mijubu wa sheria ya takwimu sura 351.

Aidha,Bakilla amesema taarifa za kaya pamoja na taarifa binafsi za wanakaya zitatolewa kwa ujumla wake kwenye ripoti ya kitakwimu,ili kuainisha hali ya soko la ajira nchini.


“Matokeo ya utafiti huu,yatasaidia kupatikana kwa viashiria mbalimbali vya takwimu za soko la ajira nchini kama;ukosefu wa ajira kwa makundi mbalimbaliya jamii,ajira isiyo timilifu,ajira katika sekta isiyo rasmi,ushiriki kazi kwa wanawake na wanaume na utumikishwaji wa watoto”,alifafanua.

No comments:

Post a Comment