Friday, February 14, 2014

Wajasirimali 40 wapata mafunzo ya usimamizi na uthibiti wa fedha.

Mratibu wa shirika lisilo la kiserikali la Mother and Children of Central Tanzania (MCCT), Everline Lyimo akitoa nasaha zake kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo wanachama wa shiriki hilo ikiwemo usimamizi na uthibiti wa fedha.
Mwezeshaji Elihuruma Hema,akitoa mafunzo ya usimamizi na uthibiti wa fedha kwa wanachama 40 wa shirika lisilo la kiserikali la Mother and children of central Tanzania (MCCT).Mafunzo hayo yalifanyikia kwenye ukumbi wa mikutano wa hotel ya Stanley mjini.
Baadhi ya wanachama wa shirika lisilo la kiserikali la Mother and Children of Central Tanzania waliohudhuria mafunzo ya usimamizi na uthibiti wa fedha yaliyofanyika kwenye ukumbi wa hotel ya Stanley mjini Singida.

WANACHAMA 40 wa shirika lisilo la kiserikali la Mother and Children of Central Tanzania (MCCT) la mkoa wa Singida wamehudhuria mafunzo ya usimamizi na uthibiti wa fedha kwa lengo wawe na uwezo mpana zaidi wa kuboresha shughuli zao za ujasiriamali.

Akizungumza na waandishi wa habari,  Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Elihuruma Hema amesema pia lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wanachama hasa wanawake, kujua taratibu za fedha kitaalam ili ziwasaidie kuendesha shughuli zao kwa ufanisi.

Amesema katika kuwajengea uwezo wanachama hao,wamefundishwa namna bora ya kuweka kumbu kumbu za fedha kwenye vitabu husika ili mwisho wa siku iwe rahisi kwao kujua wanapata faida au hasara.

 ”Kwa ujumla maisha yanahitaji mahesabu, ukisimamia vizuri mahesabu ikiwemo ya biashara ni lazima faida itapatikana.  Lakini ukifanya tofauti ikiwemo kutokutumia vitabu husika katika kuweka kumbu kumbu ya fedha vizuri utapoteza fedha bila kujijua”,alifafanua Hema.

Mkufunzi huyo amesema kutokana na ukweli huo, kila mtu au mjasiriamali anapaswa kuhakikisha
anajifunza zaidi juu ya usimamaizi na uthibiti wa fedha ili shughuli yo yote anayofanya iwe na tija zaidi.

Awali mratibu wa MCCT, Everline Lyimo amesema mafunzo hayo ni mwendelezo wa mafunzo mbali mbali wanayokusudia kuwafunza na kuwapa wanachama wao ujuzi wa matumizi sahihi ya fedha.

Alitaja mafunzo mengine kuwa ni mpango mkakati na utunzaji wamazingira.


“Tunapenda kutoa shukrani zetu za dhati kwa shirika la The Foundation for Civil Society kwa kutupa ruzuku ya zaidi ya shilingi 7.4 milioni. Ruzuku hii inatujengea uwezo sisi viongozi na wanachama wetu wa MCCT kwa kupata mafunzo mbali mbali ya kuendesha shughuli zetu ziwe za tija zaidi”,amesema Lyimo.

No comments:

Post a Comment