Monday, February 24, 2014

Halmashauri ya Manispaa ya Singida yapongezwa kwa kujenga daraja.

 Mkuu wa mkoa wa Singida, Dk.Parseko Kone,(wa kwanza kushoto) akipata maelezo kutoka mkandarasi wa daraja la Mwankoko manispaa ya Singida,Rogers Mchau(anayenyoosha mkono) juu ya maendeleo ya ujenzi wa daraja kijiji cha Mwankoko.

Dk.Kone alilikagua daraja hilo baada ya kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa, kulalamika kwamba fedha zinazotumika katika ujenzi huo ni nyingi hazifanani na daraja lenyewe. Baada ya kulikagua,alikiri kuwa daraja hilo lina thamani na fedha zilizotumika na kwamba bado kuna zaidi ya shilingi 192 milioni zinahitajika ili kukamilisha ujenzi huo.
Mkuu wa mkoa wa Singida, Dk. Parseko Kone,akikagua ujenzi wa daraja la kijiji cha Mwankoko manispaa ya Singida.
Mkuu wa mkoa wa Singida, Dk.Parseko Kone, akitoa maelekezo juu ya kuboresha ujenzi wa daraja la kijiji cha Mwankoko manispaa ya Singida.
 Daraja la kijiji cha Mwankoko linaloendelea kujengwa na mkandarasi Rogers Mchau.
Mkuu wa mkoa wa Singida (kushoto) akizungumza na Meya Mstahiki wa manispaa ya Singida,Sheikh Salum Mahami wakati alipokuwa akimaliza kukagua ujenzi wa daraja la kijiji cha Mwankoko.
MKUU wa mkoa wa Singida,Dk.Parseko Kone,ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Singida,kwa juhudi zake za kujenga daraja linalolingana na thamani ya fedha iliyotumika.

 Dk.Kone ametoa pongezi hizo mwishoni mwa wiki wakati akikagua ujenzi wa daraja hilo, ulioanza rasmi desemba 12 mwaka 2011 na ulitarajiwa kukamilika novemba 14 mwaka 2012.Daraja hilo linaunganisha kata ya Mwankoko na kata ya Mtamaa.

Amesema kuwa fedha ambayo imetumika hadi sasa ya zaidi ya shilingi 216.1 milioni,thamani ya fedha hiyo inafafanana kabisa na kazi ya ujenzi iliyofanyika.

 “Kwa kweli mmefanya kazi nzuri pamoja na mkandarasi wenu.Fedha ambazo mmeziomba serikali kuu ili mmalizie ujenzi wa daraja hili,tutakuwa nyuma yenu katika kuhakikisha mmezipata,ili ujenzi uweze kukamilika kwa mujibu wa mkataba wenu”,amesema.

Mapema Mkurugenzi wa Manispaa hiyo,Joseph Mchina,amesema mradi huo wa ujenzi wa daraja hilo,fedha zake zimetoka katika mfuko wa barabara kupitia OWM-TAMISEMI,zikiwa ni fedha za maombi maalum ya ujenzi wa madaraja.

 Katika hatua nyingine,Mchina amesema hadi sasa ujenzi huo wa daraja,
umekamilika na magari yameanza kulitumia kwa tahadharai,kwani bado kuna kazi ambazo hazijakamilika.

 Mkurugenzi huyo alitaja baadhi ya kazi ambazo bado hazijakamilika kuwa ni ujenzi wa barabara ya kuingia na kutoka,mifereji ya wazi kandokando ya barabra ya kuingia na kutoka na kuweka alama barabarani.

 Alitaja kazi zingine ambazo bado hazijakamilika,kuwa ni pamoja na kazi ya ujenzi wa kuta za kulinda daraja,kuweka bomba za pembeni na kuweka nguzo za kuonesha mwlekeo wa daraja.

 “Katika mwaka wa fedha wa 2014/2015,halmashauri ya manispaa,imeomba kiasi cha shilingi 200 milioni kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu”,amesema.


Mkuu huyo wa mkoa,amelazimika kukagua mradi huo wa ujenzi wa daraja,baada ya ujenzi huo kulalamikiwa kuwa umetumia fedha nyingi ambazo hazilingani na kazi iliyofanyika.Mbaya zaidi ni kwamba ujenzi huo upo nyuma ya muda kwa mujibu wa mkataba.

No comments:

Post a Comment