Thursday, February 20, 2014

TRA Singida yapandisha Kizimbani Wafanyabiashara.

Jengo la ofisi kuu mamlaka ya mapato (TRA) mkoa wa Singida iliyopo mjini Singida.

MAMLAKA ya Mapato nchini (TRA) Mkoa wa Singida imewapandisha kizimbani wafanyabiashara wanne wa mjini Singida kwa makosa mbalimbali, ikiwemo kutotumia kwa makusudi mashine za kieletroniki (EFD) kukusanyia kodi, huku wakijua wazi ni kosa kisheria.

Shitaka lingine linalowakabili wafanyabiashara hao akiwemo Sabra Mohammed na Khalfani Juma ni kushindwa kulipa kodi ya VAT kwa makusudi, katika vipindi tofauti tofauti kati ya mwezi februari mwaka jana hadi januari mwaka huu, jambo ambalo ni kinyume cha sheria ya TRA, kifungu namba 148 cha mwaka 2008.

Mbele ya hakimu mfawidhi wa mahakama ya mkoa Singida Joyce Minde, ilidaiwa na afisa sheria mwandamizi wa TRA kanda ya kaskazini Geva Masele kuwa, wakati washitakiwa wakiendelea na biashara zao katika eneo la barabara ya Karume mjini Singida, walifanya makosa hayo na hivyo kuikosesha serikali mapato.

Hata hivyo washitakiwa wote walikana mashitaka yao na wapo nje kwa dhamana ya Sh. Milioni mbili kila mmoja kuwa na mdhamini mmoja na shauri hilo litatajwa tena februari 26 mwaka huu.

Wakati huo huo Robert Mkoma anayefanya biashara zake katika barabara ya Lumumba mjini Singida, amefikishwa mbele ya hakimu mkazi wilaya Singida Flora Ndale, kwa shitaka la kushindwa kulipa
kodi na kutotumia mashine ya kietroniki (EFD) kwa makusudi, jambo ambalo ni kosa kisheria.

Ilidaiwa na afisa sheria mwandamizi wa TRA Kanda ya kaskazini Masele kuwa, mshitakiwa alifanya makosa hayo kati ya julai mwaka hadi januari mwaka huu. Hata hivyo mshitakiwa huyo alikana makosa hayo na yupo nje kwa dhamana ya Sh.Milioni moja hadi februari 26 mwaka huu, kesi yake itakapotajwa tena.

Katika shauri lingine, TRA imempandisha kizimbani Rufina Kundya mbele ya hakimu Asha Mwetindwa wa mahakama ya hakimu mkazi mjini Singida kwa kosa la kushindwa kulipa kodi na kutotumia kwa makusudi mashine ya kieletroniki (EFD), hali ambayo anaikosesha serikali mapato.

Masele aliieleza mahakama kuwa, mshitakiwa huyo alifanya kosa hilo kati ya februari mwaka jana hadi januari mwaka huu mjini Singida. Mshitakiwa huyo naye alikana kosa hilo na yupo nje kwa dhamana ya Sh. Milioni moja na shauri hilo litatajwa tena siku ya fenruari 27 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment