Tuesday, February 11, 2014

Wawili wapoteza maisha katika ajali ya basi la Zuberi.

WASOMAJI WETU TUNAOMBA RADHI KAMA UTAKWAZIKA NA PICHA ZIFUATAZO.
Mtoto mmoja aliyelalaliwa na kusababisha kifo chake na basi la Zuberi T.119 AZZ lilokuwa likitokea Mwanza kuelekea jijini Dar-es-salaam na kupinduka katika eneo la kijiji cha Tumaini kata ya Issuna wilaya ya Ikungi wakati likimkwepa bibi aliyekuwa akikatisha barabara.
 Mmoja wa majeruhi akiwa amelazwa katika Hosptali ya Mkoa ya Singida.
 Mmoja wa majeruhi akiongea na waandishi wa habari katika Hospitali ya mkoa mjini Singida.

BASI la kampuni ya Zuberi T.119 AZZ lililokuwa linatokea jijini Mwanza likielekea jijini Dar-es-salaam,limepinduka na kusababisha vifo vya abiria  wawili na kujeruhi vibaya wengine arobaini wakati likimkwepa bibi mmoja aliyekuwa anakatisha barabara.

 Ajali hiyo imetokea jana saa 7.30 mchana katika barabara kuu ya Sindida –Dodoma eneo la kijiji cha Tumaini kata ya Issuna wilaya ya Ikungi mkoani Singida.

Afisa wa makosa ya jinai mkoa wa Singida (RCO), Thobias Sedoyeka amesema kuwa basi hilo lililokuwa likiendeshwa na Fadhili Kalembo (35),lilipofika eneo la tukio,bibi mmoja alijitokeza akiwa anavuka barabara.

Amesema dereva wa basi alijitahidi kumkwepa bibi huyo lakini ghafla bibi alirudi tena barabarani kitendo kilichosababisha basi hilo kupinduka na kuserereka hatua zaidi ya 50 wakati likimkwepa kwa mara ya pili.

 “Basi hili lilimlalia mtoto mdogo ambaye
aliweza kutolewa baada ya basi la Zuberi kunyanyuliwa na wichi ya lori ambalo lilikuwa linapita katika barabara hiyo”,amesema.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa hospitali ya mkoa ya mjini Singida, Deogratus Banuba amesema kuwa wamepokea maiti moja iliyotokana na ajali ya basi la Zuberi na kwamba bado wanaendelea kusubiri mwili wa mtoto aliyefia eneo la ajali.

 “Kwa upande wa majeruhi,tumepokea majeruhi 40 ambao wameumia vibaya sehemu mbalimbali ya miili yao ikiwemo kuvunjika mikono na miguu.Kati yao wanne,mikono yao imesagika vibaya na tumejitahidi kuirudisha katika hali yake”,amesema Dk.Banuba.

Amesema kuwa majeruhi wengine wanne,wao wamewapa  rufaa ya kwenda hospitali ya KCMC Moshi mjini mkoa wa Kilimanjaro.

No comments:

Post a Comment