Wednesday, February 5, 2014

Chadema kuendelea kuwavua uanachama viongozi mamluki.

Baadhi ya wakazi wa mji wa Singida,wakipokea helkopta iliyombeba mwanasheria wa CHADEMA, Tundu Lissu,ambaye alihutubia kwenye uwanja wa Ukombozi mjini Singida.
Mwanasheria wa CHADEMA Tundu Lissu,akihutubia mamia ya wakazi wa mji wa Singida katika operation ya kuimarisha chama hicho.Mkutano huo ulifanyika katika uwanja vya Ukombozi mjini Singida.

Baadhi wa wakazi wa Singida mjini,wakimsikiliza mwanasheria wa CHADEMA Tundu Lissu, wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Ukombozi mjini Singida.

MWENYEKITI wa Baraza la Vijana Taifa (BAVITA), John Heche amesema Chadema kitaendelea kuwavua uanachama kiongozi au mwanachama  yeyote, pindi anapobainika kusaliti ustawi wa chama hicho.

Heche aliyasema hayo hivi karibuni wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa ukombozi mjini hapa.

Amesema CHADEMA kamwe haitawalea wasaliti kama CCM ambayo inalea mafisadi na mawaziri mizigo,itaendelea kuwavua uanachama wasaliti bila kujali umaarufu wa mtu au kiongozi.

 “Kelele zimepingwa sana kwamba CHADEMA sasa kinakufa kisa eti Zitto Kabwe,amevuliwa nafasi zake zote za uongozi.Wanasingida,hivi kweli CHADEMA ife kwa sababu ya mtu mmoja tu.Haitatokea kabisa”,amesema na kuongeza;

 “Viongozi wote mashuhuri hivi sasa kwenye chama cha CHADEMA,hata wakiondoka,chama kitabaki pale pale na hakitaterereka.Hakuna kiongozi au mwanachama ambaye yupo juu ya CHADEMA,kwa hiyo sisi viongozi tutaondoka,lakini CHADEMA itabaki pale pale”,alisisitiza Mwenyekiti huyo.

Heche amesema CHADEMA ikichukua dola,haitawalinda mafisadi au viongozi mizigo kama inavyofanya CCM,CHADEMA itawafukizia mbali na endapo kutakuwa na adhabu ya kuwanyonga hadi wafe,adhabu hiyo itatekelezwa bila ubishi.

Kwa upande wake Mwanasheria wa CHADEMA,Tundu Lissu amewataka Watanzania mwakani (2015),kuchagua
rais mwadilifu na sio anayehonga mapadre fedha chafu zilizotokana na ufisadi.

Akifafanua,amesema baadhi ya viongozi hivi sasa wanapita kwenye nyumba za ibada kutoa rushwa na kudai kwamba zamu yao ya kuwa rais,imewadia.


“Watanzania wenzangu,kiongozi au mtu ye yote anayetaka urasi kwa kuhonga fedha za ufisadi huyo hatufai tunataka raisi ajaye awe ni mtu mwadilifu na mwenye uchungu wa kweli na Tanzania”,amesema Tundu.

No comments:

Post a Comment