Sunday, September 29, 2013

Mtoto auawa na Bibi yake kwa kuchelewa kuleta Mwiko wa Ugali

 Mwenyekiti wa mtaa wa Lulumba New Kiomboi mjini wilaya ya Iramba, Abel Seit akitoa taarifa kwa waandishi wa habari (hawapo kwenye picha) juu ya tukio la mtoto wa kike Zuhura (6) kumwagiwa maji ya moto na bibi yake Magreth Sombi (55) na kusababisha kifo chake.
 Mwenyekiti wa mtaa wa Lulumba New Kiomboi mjini wilaya ya Iramba,Abel Seit akifungua mlango wa nyumba ya Magreth Sombi ambaye kwa sasa anashikiliwa na polisi kwa tuhuma ya kumuuguza mjukuu wake Zuhura na kusababisha kifo chake.
 Sehemu ya ndani ya nyumba ya mtuhumiwa Magreth Sombi anayedaiwa kumuuguza mjukuu wake maji ya moto na kusababisha kifo chake.
 Mtoto wa mtuhumiwa Magreth Sombi,Naomi ambaye hivi karibuni amehitimu mafunzo ya ualimu mkoani Tabora na alikuwa anasubiri kupangwa kazi.Kwa sasa Naomi na mama yake Magreth Sombi wanashikiliwa na jeshi la polisi wilaya ya Iramba kuhusiana na mauaji ya Zuhura.
Picha ya mtuhumiwa Magreth Sombi anayetuhumiwa kumuua mjukuu wake Zuhura kwa kumumwagia maji ya moto ambayo yaliyokuwa yatumike kupikia ugali wa jioni.

Mtoto wa kike aliyetambulika kwa jina moja la Zuhura (6) mkazi wa mtaa wa Lulumba New Kiomboi mjini, wilayani Iramba,amefariki dunia baada ya kudaiwa kuuguzwa kwa maji ya moto na bibi yake Magreth Sombi (55).

Imedaiwa kwamba Zuhura alimwagiwa maji ya moto ambayo yalikuwa yatumike kupikia ugali,kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kitendo cha mtoto huyo kuchelewa kukabidhi mwiko aliotumwa na bibi yake.

Akisimulia mkasa huo wa aina yake,Mwenyekiti wa mtaa wa Lulumba,Abel Seit,amesema tukio hilo limetokea Septemba 24 mwaka huu majira ya jioni huko mtaa wa Lulumba katika mji wa New Kiomboi.

Amesema siku ya tukio,Zuhura alitumwa na bibi yake Magreth akalete mwiko wa kusoga ugali wa jioni na inadaiwa kwamba mtoto huyo alichelewa kuukabidhi mwiko huo.

Seit amesema baada ya kuleta mwiko huo,alimwagiwa mwilini maji yaliyokuwa yamechemka tayari kwa kutumika kupikia ugali wa jioni.

“Kama vile adhabu hiyo haikutosha,Magreth kwa ushirikiano na mtoto wake Naomi,walimkamata kwa nguvu Zuhura na kisha kuingiza viganja
vyake vya mikono yote ndani ya sufuria iliyokuwa ina maji yaliyokuwa yamechemka kwa kiwango cha juu.Mtoto Zuhura aliweza kuugua na nyama zote kutoka na kubakia mifupa”amesema kwa masikitiko mwenyekiti huyo.

Seit amesema Zuhura alifariki dunia Septemba 25 akiwa anapatiwa matibabu katika hospitali ya wilaya ya Iramba.

“Baada ya muda mrefu kupita baada ya Zuhura kufariki dunia,bibi yake Magreth alimtuma mtoto wake Naomi kuja nyumbani kwangu kunipa taarifa hiyo.Cha ajabu ni kwamba hawakupiga yowe wala kutoa taarifa kwa majirani zao”,amesema na kuongeza;

“Nilipomhoji ni kwa nini hajawajulisha majirani zao juu ya kifo hicho,kwanza alinionya kwamba nisije nikawaambia watu wala majirani kwa sababu hataki watu wajue au waje warundikane kwake na kwamba mwili wa Zuhura wakati wo wote utachukuliwa na wazazi wake kwenda kuzika Singida mjini”. 

Kwa upande wake jirani wa karibu wa Magreth,Elieza Mgwali,amesema Zuhura ambaye ana miezi miwli toka aanze kuishi na bibi yake,aliishi kwa mateso makubwa.

“Mtoto huyu ameteseka mno toka aanze kuishi na bibi yake,alifanyishwa kazi ambazo ziko nje ya uwezo wake na mara nyingi alikuwa akinyimwa hata chakula.Mara nyingi tu tulikuwa tunashitukia anaingia kwetu na kwenda moja kwa moja jikoni na kujichukulia chakula bila hata kuomba.Kwa sababu tuliisha tambua mateso yake,tulikuwa tukimruhusu ale hadi ashibe”,alisema.

Majirani wa Magreth wamepigwa butwaa kutokana na kitendo hicho kufanywa na mama ambaye alikuwa hakosi kanisani na alikuwa mwimbaji mzuri wa kwaya.”Kumbe chui aliyekuwa amevaa ngozi ya kondoo”,alisikika mama mmoja ambaye alidai kuwa walikuwa wakisali na Magreth.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa mtaa,Magreth na mtoto wake Naomi,wanashikiliwa na polisi kuhusiana na mauaji hayo.


Juhudi kubwa zimefanywa na mwandishi wa habari hii kupata undani wa mauaji hayo,hazijaa matunda baada ya kumpigia Kamanda wa Polisi mkoa wa Singida kupitia namba yake ya simu ya mkononi kuita bila kupokelewa na hata meseji ilipotumwa nayo haikuweza kujibiwa.

No comments:

Post a Comment