Tuesday, February 25, 2014

Mbaroni kwa mauaji ya makusudi ya kitoto kichanga.

 
Kamanda wa Polisi mkoa wa Singida, SACP Geofrey Kamwela.

JESHI la Polisi mkoani Singida linamshikilia Naomi Daud (20) mkazi wa kitongoji cha Mahawa kata ya Mungumaji tarafa ya Unyambwa Manispaa ya Singida kwa tuhuma ya kumuuawa mtoto wake mara baada ya kujifungua.

Imedaiwa Naomi baada ya kujifungua,alimnywesha mtoto wake maji ya mvua lita moja na kusababisha kifo chake papo hapo.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Singida,SP.Cordula Lyimo amesema tukio hilo la kusikitisha limetokea februari nne mwaka huu usiku wa nane huko katika kata ya Unyambwa Manispaa ya Singida.

Amesema siku ya tukio,Naomi akiwa chumbani kwao na mama yake mzazi,alijifungua bila kusaidiwa na mtu na mama yake alikuwa akiangalia kitendo hicho kama sinema.

“Mara baada ya kumaliza kujifungua,mtuhumiwa aliweza kumnywesha kichanga hicho
maji ya mvua lita moja.Maji hayo ya mvua yalitokana na mvua iliyokuwa ikinyesha kwa wakati huo.Kichanga hicho baada ya kulazimishwa kunywa maji hayo,alianza kutapika na haikuchukua muda alifariki dunia”,amesema.

Kaimu Kamanda huyo amesema Naomi na mama yake mzazi waliweza kushinda na maiti hiyo kwa siku nzima na siku iliyofuata saa mbili usiku waliibeba maiti hiyo na kwenda kuitupa kichakani eneo la umbali wa kilomita tatu kutoka wanakoishi.

“Kukamatwa kwa binti huyo kunatokana na tukio la kuokotwa kwa mtoto mchanga akiwa amefariki dunia februari 12 saa mbili asubuhi katika eneo la Bomani mjini hapa.Mwili wa kichanga hicho kilitelekezwa na mwanamke asiyefahamika”,amesema.

Hata hivyo,amesema baada ya uchunguzi kufanyika,raia wema waliweza kutoa taarifa zilizoweza kusaidia kukamatwa kwa mtuhumiwa Naomi.

Kaimu Kamanda huyo,amesema baada ya upelelezi kukamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma inayomkabili.

No comments:

Post a Comment